March 24, 2014





Wakati kikosi cha Simba kikiwa kwenye harakati zake za kuhakikisha kinafanya vizuri katika mechi zake za ligi kuu zilizobakia, beki wa kati wa timu hiyo raia wa Kenya, Donald Musoti, amewataka wachezaji wenzake kudumisha  umoja na upendo ili waweze kutimiza lengo hilo.

Hata hivyo, amewataka kuachana na tabia ya kujigawa katika makundi ambayo yanaweza kusababisha mpasuko ndani ya timu hiyo kwa hivi sasa na badala yake wawe kitu kimoja kwa kila jambo linalohusu timu.

Musoti alisema hali ya umoja na upendo iliyopo kwa sasa katika kikosi hicho ni ya kawaida na inatakiwa kudumishwa zaidi kwa wakati huu ambao timu hiyo ipo kwenye vita kali ya kutafuta nafasi ya pili.

Alisema tangu afike katika kikosi hicho, amekuwa akifurahia maisha lakini jambo linalomsikitisha ni kutokuwepo kwa upendo wa dhati kati ya wachezaji pamoja na benchi lao la ufundi,  hali ambayo anaomba ifanyiwe kazi.

“Viongozi nao wanatakiwa kuwa kitu kimoja kwa sasa na kusahau tofauti zao ambazo walikuwanazo huko nyuma, hivi sasa tunahitaji kuhakikisha tunamaliza ligi kuu tukiwa katika nafasi nzuri itakayotuwezesha mwakani kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa.

“Hata hivyo, lengo hilo litatimia pale watu wote wa Simba tutakapokuwa kitu kimoja, kwani nafasi bado tunayo,” alisema Musoti.

Kabla ya mchezo wa jana Jumapili dhidi ya Coastal Union, Simba ilikuwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 36 ambazo ni sita nyuma ya Mbeya City iliyo katika nafasi ya tatu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic