Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Ben
Mwalala, amewataka Yanga kujipanga vizuri kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi
ya Al Ahly itakayopigwa nchini Misri Jumapili ijayo.
Mwalala ameliambia gazeti hili kuwa, ili
Yanga waweze kufanya vizuri katika mechi hiyo, wachezaji wote wanatakiwa
kucheza kwa nguvu bila ya kutegeana kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho.
Alisema katika mechi ya juzi iliyochezwa
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, kuna baadhi ya wachezaji walikuwa hawatekelezi
majukumu yao ipaavyo, ndiyo maana kuna wakati Al Ahly walionekana kutawala
mchezo huo.
“Waliokuwa wanapambana muda wote
walikuwa ni Frank Domayo, pamoja na safu ya ulinzi, hao walikuwa wanakaba mwanzo
mwisho lakini wengi waliobakia walikuwa hawafanyi majukumu yao kama
inavyotakiwa.
“Hivyo basi katika mechi ya marudiano
watu wote wanatakiwa kupambana na kukaba kwa nguvu ili kuhakikisha wanaibuka na
ushindi kwenye mechi hiyo,” alisema Mwalala ambaye alikuwepo katika kikosi cha
Yanga kilichochapwa jumla ya mabao 4-0 na Al Ahly mwaka 2009, Dar wakipigwa moja
na ugenini 3-0.
0 COMMENTS:
Post a Comment