Beki wa kati wa Coastal Union ya jijini
Tanga, Juma Nyosso, amesema hadi sasa hajui kama ataendelea kuichezea timu hiyo
msimu ujao kwa kuwa bado hajafanya maamuzi.
Nyosso alisajiliwa na Coastal Union mwanzoni
mwa msimu huu akitokea Simba. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa
msimu.
Nyosso amesema kila mtu ana akili yake
kichwani mwisho wa ligi kutokana na kile kinachotokea klabuni hapo hivi sasa na
kudai kuwa kwa sasa anaangalia jinsi ya kuisaidia timu yake hiyo lakini kuhusu
kuongeza au kutoongeza mkataba, anasubiri hadi mwisho wa msimu ndiyo aamue.
“Lengo letu ni kuhakikisha timu yetu
inamaliza katika nafasi ya nne kwenye ligi kwani kila mmoja anaangalia nafasi ya
timu jinsi ilivyo ili tuweze kuisaidia kusonga mbele zaidi.
“Ligi ni ngumu, ina ushindani mkubwa na
wala haitabiriki, kila timu inahitaji kumaliza katika nafasi nzuri.
“Kuhusu kuongeza au kutoongeza mkataba,
nasubiria hadi msimu uishe ili niweze kutoa maamuzi kwa kuwa mkataba wangu
unatarajiwa kufikia tamati mwishoni mwa ligi, kila mtu akili kichwani mwake
kutokana na kile kinachoendelea hivi sasa,” alisema Nyosso.
Coastal juzi ilikumbana na kipigo cha
mabao 4-0 kutoka kwa Azam na kuzidi kujichimbia katika nafasi ya saba kwenye
msimamo wa Ligi Kuu Bara.
0 COMMENTS:
Post a Comment