Na Saleh
Ally
MARA kibao
umesikia mashabiki wa Yanga na Simba wakichapana kwa madai kuwa mmoja wao
amekiuka na kuvuka upande na kuingia upande wao akiwa na rangi ambazo si zao.
Yanga
wanatumia kijani na njano, Simba ni nyekundu na nyeupe. Mashabiki na wanachama
wa timu hizo wanazitumia kama msingi wa itikadi ya kila upande.
Inawezekana
wako sawa au si sawa kwa kuwa rangi hizo si mali ya Yanga au Simba na
zinatumika kwenye vitu vingi sana, kama bendera ya mataifa, makampuni na sehemu
nyingine.
Ili
kuthibitisha hii ni Yanga au Simba, kama hata ikiwa ni njano, kijani, nyekundu
na nyeupe, bado suala la nembo au maneno ndiyo yanapaswa kuwa uthibitisho tu.
Azam FC imekuwa
ikifanya vizuri kwa misimu mitatu sasa, inaonyesha ni moja ya timu bora na
mwenendo wake kwenye Ligi Kuu Bara sasa unathibitisha hilo.
Lakini
imekwama kwenye rangi, Azam FC bado haijajitambulisha kwa rangi rasmi, kwamba
inatumia rangi fulani na ikionekana angalau bila nembo unaweza kusema hii ni
timu fulani.
Mbeya City ambayo
pamoja na kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara ukiwa ndiyo msimu wake wa Ligi
Kuu Bara, imekuwa tofauti kwa kuwa imeweza mapema.
Mbeya City
imeweza kujitambulisha katika msimu wa kwanza tu kupitia uwezo na sasa rangi ya
jezi. Kama utavaa rangi ya zambarau na nyeupe, basi moja kwa moja unaonekana
wewe ni mnazi wa Mbeya City.
Tayari
wamefanikiwa kuichukua rangi hiyo ya zambarau katika msimu wa kwanza tu na
ndiyo inayoshika nafasi ya tatu sasa kwa umaarufu baada ya njano na nyekundu
ambazo zimekuwa zikichukuana tokea mwaka 1936 ilipozaliwa Simba.
Zambarau
ilikuwepo, hakuna timu iliyotamani kuitumia na badala yake kijani na blue ndiyo
zilikuwa zikigombewa na timu nyingine. Miaka minne iliyopita, African Lyon
ikajitahidi na kuanza kutamba na rangi ya machungwa.
Pamoja na
kuonyesha utofauti katika suala la rangi na muonekano mpya, lakini African Lyon
ilishindwa kufanya vizuri na kupata umaarufu katika rangi za jezi zake kwa kuwa
karibu misimu yote ilikuwa ikipambana isiteremke daraja.
Mambo
yamekuwa tofauti kwa Mbeya City inayoongozwa na Juma Mwambusi. Hadi sasa ni
kati ya timu zinazowania kutwaa ubingwa au kushika nafasi ya pili ambayo inatoa
nafasi kwa timu kushiriki Kombe la Shirikisho.
Uimara wa
Mbeya City bila ya kujali kuwa ni wageni wa Ligi Kuu Bara na wanashiriki kwa
msimu wa kwanza umeifanya ijenge uimara wa soko lake.
Soko la
jezi za Mbeya City ziko katika nafasi ya tatu kwa sasa. Ndizo jezi zinazouzika
au kutazamwa sana baada ya zile za Yanga na Simba.
Tayari
Mbeya City imeweza kuuza hadi jezi 10,000, kitu ambacho si kidogo. Ingawa wako
wanaosema zimeuzwa zaidi, hata kama fedha bado haijaingia kwenye klabu. Bado
inaonyesha klabu hiyo ya Mbeya imeishajenga msingi wa soko.
Tayari
inaweza kufanya biashara, maana yake kama wataingia kwenye soko la vifaa, basi
wana kila sababu ya kufanya vizuri hata kuliko Azam FC ambao wana uwezo kifedha
na wamekuwa kitambo katika ligi kuu kuliko wao.
Nini
nilichowafanya wafanikiwe? Jibu ni mambo mawili tu. Uwezo wa kazi yao
waliouonyesha katika Ligi Kuu Bara na pili ni sapoti kutoka kwa mashabiki wao
ambao wameonyesha wazi wanakubaliana na timu yao inachokifanya, wakawa
wazalendo, wakajitolea katika michango na kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono.
Mbeya City
kwa sasa iko katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa
imepiga mechi 21 na kati ya hizo imepoteza mbili tu.
Katika
mechi hizo, Mbeya City imeonyesha ni kati ya vikosi bora kwa kuwa imefunga mabao
27 na kufungwa 17. Imefanikiwa kushinda mechi 10 na imepata sare 9.
Kama
utafanya ubora wa viwango kutokana na kufunga, kufungwa, sare na mabao ya
kufunga na kufungwa, Mbeya City iko katika tatu bora ya Ligi Kuu Bara.
Ndiyo
inaonekana kuwa ‘tatizo’ kwa Simba kupanda katika nafasi hiyo, lakini hofu kwa
Yanga na Azam FC kwamba inaweza kuwapokonya nafasi na kuvuruga hesabu zao.
Yanga na
Azam FC wanachuana kileleni lakini macho ya wote wawili ni kwa Mbeya City kwa
kuwa mwendo wao ni sawa na wale watu “wanaomfukuza mwizi kimyakimya.”
0 COMMENTS:
Post a Comment