March 9, 2014


Mechi ya leo kati ya wenyeji dhidi ya Al Ahly ni ngumu na matokeo yote matatu yanaweza kupatikana katika mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ya kuwania kucheza 16 bora.

Yaani kushinda, sare au kupoteza kwa timu yoyote mbili kati ya hizi kwa kuwa kila upande unaonekana kuuchukulia mchezo huu kwa kiwango cha juu sana kuwa ni muhimu.
Yanga tayari wameonja utamu wa ushindi, bila ya shaka yoyote wanataka kuimalizia kazi yao. Al Ahly wamefanya makosa na kuruhusu kufungwa bao 1-0 jijini Dar es Salaam, wanachotaka sasa ni kurekebisha na kushinda leo.
Hakuna timu imefanya mzaha hadi leo hii ya mechi, hii inaonyesha kiasi gani kila upande unataka kuhakikisha unasonga mbele, Al Ahly kutoka nyuma na Yanga kumalizia kazi.
Yoyote kati yao anaweza kusonga mbele kutegemeana na namna gani amezicheza karata zake. Yanga wanajua mipango ya Warabu na inaonyesha hakutakuwa na mzaha.
Al Ahly wana kikosi bora, hakuna haja ya kuwadanganya Yanga wala asitokee mtu akasema wameisha, inawezekana wameshuka kiwango lakini hawajaondoka kwenye kiwango bora.
Nani unaweza ukamwambia akakuelewa, kwamba tokea wachukue ubingwa wa Afrika si chini ya miezi sita iliyopita, sasa itakuwaje leo kiwango chao kiwe kimeshuka hadi kuwa wabovu. Hilo haliwezekani.
Pima kiwa walichokionyesha Dar es Salaam katika mechi ya kwanza dhidi yao, kama ingekuwa ni timu lainilaini, basi wangefungwa hata mabao saba. Lakini haikuwa hivyo.
Safari hii wanacheza nyumbani kwao, wana mbinu zao za nyumbani. Ingawa kama Yanga wamejipanga vizuri hauwezi kusema hawafungiki, ndiyo maana ya soka.

Hadi sasa ndiyo timu bora namba moja barani Afrika, tunatambua kuna timu ngapi katika bara hili. Hivyo kuwaambia Yanga Al Ahly wamekwisha ni sawa na kuwadanganya waweke jicho kwenye tundu la bunduki kwa madai imekwisha risasi, kumbe sivyo.

Kikubwa kama ambavyo wameanza, Yanga lazima waende wakiamini mchezo ni mgumu na hakutakuwa na mzaha hata chembe, wapambane kiume kweli tena kwa dakika 90.

Simba walifanya kosa dhidi ya timu ya Warabu kutoka Algeria, unakumbuka walichezea jijini Cairo na wakaweza kuhimili mikiki hadi dakika tano za mwisho wakafungwa mabao matatu.

Soka dhidi ya Al Ahly ni dakika 90, ndiyo unaweza kusema umepata ushindi au mambo yamekwenda vizuri. Nidhamu ya mchezo yaani kufuata maekelezo ya kocha ni jambo jema kwao.

Utaona namna Yanga baada ya kufika hapa, Al Ahly walionyesha uungwana kupindukia. Lakini hawakuwa na maana hiyo badala yake walitaka kuwasogeza karibu ili waweze kuwamaliza kilahisi.
Inaonekana Yanga walishituka na kuachana nao, wakajificha na kukaa mbali. Walipofika hapa pia wakafanya kama Cairo wakapanga hoteli kwa juhudi zao wenyewe zilizoongozwa na Makamu Mwenyekiti wao Clement Sanga.

La nje ya uwanja limewezekana, lakini bado kuna ndani ya uwanja. Pale ndiyo fainali na kuna mambo mengi sana na kama Yanga hawatakuwa makini maana yake hakuna watakachokuwa wamefanya kuanzia mwanzo.
Lazima Al Ahly watahamishia nguvu uwanjani baada ya kukwama kila sehemu. Watakachotaka kufanya ni kucheza kwa kiwango bora lakini hata hujuma watakuwa tayari, wanachotaka ni kushinda.
Mfano kujiangusha wapate penalty, kujiangusha wapate mikwaju ya adhabu kwa kuwa wana wapigaji wazuri, yote ni mambo muhimu ya wao Yanga kujifunza mapema, ninaamini wamefanya.

Lakini waende wakijua mechi si lahisi, mashabiki wa Yanga na Watanzania ambao wameonyesha uzalendo wanapaswa kujua Yanga wana kazi ngumu na matokeo yataamuliwa na wao. Iwapo wanataka kushinda, lazima wakubali kufanya kazi ngumu lakini kwa mipango na umakini mkubwa kama walivyoanza.
Namaliza hii tathmini yangu kwa kusema hivi; Yanga inaweza kuifunga Al Ahly, lakini Al Ahly inaweza kuifunga Yanga.

Kila la kheri.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic