Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga wameibuka usingizini na
kufanikiwa kushinda mabao 3-0 dhidi ya Rhino Rangers katika mechi ya Ligi Kuu
Bara kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, leo.
Yanga ambayo iliandamwa na sare mfululizo dhidi ya Mtibwa
Sugar na Azam FC ilipata bao la kwanza katika kipindi cha kwanza na mawili
kipindi cha pili.
Jerry Tegete alianza kuifungia Yanga katika dakika ya 30
baada ya kipa kushindwa kulidaka vizuri shuti la Mrisho Ngassa.
Tegete tena alipiga shuti kali katika dakima ya 67 na beki Labani
Kambole aliusindikiza wavuni wakati anajaribu kuokoa.
Wakati Rhino wanajitahidi kujitutumua, Yanga ilipata bao la
tatu katika dakika ya 90 kupitia Hussein Javu.
Pamoja na kufunga mabao hayo matatu, bado Yanga walipoteza
nafasi nyingine nyingi za kufunga kama ilivyotokea katika mechi zao mbili
zilizopita za Ligi Kuu Bara.
0 COMMENTS:
Post a Comment