Baada ya kutawala kwa taarifa za kutojulikana alipo beki wa Yanga, Kelvin
Yondani huku baba yake mzazi, mzee Patrick Yondani akikiri
juu ya hilo, mchezaji huyo amerejea kikosini na kujiunga na msafara ulienda
Arusha kucheza mechi dhidi ya JKT Oljoro.
Yondani japokuwa amesafiri na timu hiyo lakini kuna kila dalili kuwa
mchezaji huyo anaweza asicheze kutokana na kutofanya mazoezi na timu yake kwa
wiki mbili.
Hata hivyo kocha wa timu hiyo Mholanzi Hans van Plujim, huwenda akampa
nafasi kutokana na nahodha na beki wa kikosi hicho Nadir Haroub ‘Canavaro’,
kuwa na kadi tatu za njano ambazo zinamfanya kukosa mechi moja.
Yondani alitoweka Yanga baada ya kutuhumiwa kuwa amefungisha kwenye
mechi dhidi ya Mgambo Shooting iliyopigwa kwenye dimba la Mkwakwani, Tanga
Machi 30, mwaka huu.
Katika mchezo huo Yanga ilikubali kichapo cha mabao 2-1, huku ikicheza
na timu iliyokuwa na wachezaji kumi baada ya Mohamed Neto, kutolewa kwa kadi
nyekundu iliyozua sintofahamu.
Tangu alipotoweka katika kikosi hicho Yondani amekosa michezo miwili,
ambayo ni ule dhidi ya Tanzania Prisons uliopigwa Taifa, huku timu yake
ikishusha kipigo cha paka mwizi kwa kuwafunga Wajelajela kutoka mkoani Mbeya
5-0.
Pia aliikosa mechi dhidi ya Kagera Sugar ambao ulichezwa kwenye uwanja
huo na mabingwa watetezi kupata ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya Wakatamiwa hao
kutoka Kagera.
Yondani analalamikiwa kwa kutokuwa makini na kusababisha mkwaju wa penalti ulioimaliza Yanga dhidi ya Mgambo Sugar.
Lakini rafiki yake wa karibu amekuwa akisisitiza kuwa suala hilo linamuumiza Yondani kwa kuwa alikuwa katika juhudi za kutaka kuokoa.
0 COMMENTS:
Post a Comment