April 18, 2014


 Na Saleh Ally
UKIZUNGUMZIA mafanikio, Steven George Gerrard ana makubwa na amebeba makombe mengi kama lile la FA, Kombe la Ligi, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Uefa, Super Cup na mengine kadhaa.

Si mafanikio kidogo, lakini nahodha huyo wa Liverpool, hajawahi kulibeba la Ligi Kuu ya England ‘Premiership’ ambalo kama atafanikiwa kufanya hivyo msimu huu itakuwa ni mara yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 33.


Miaka 33 katika soka, tayari mchezaji anastahili kuitwa babu, ni umri ambao umemtupa mkono, lakini matendo ya Gerrard ni tofauti na umri wake na hasa katika msimu huu wa 2013-14 unaoendea ukingoni.

Ameonyesha kiwango cha juu na ndiye mchezaji mkongwe mwenye umri wa zaidi ya miaka 30 ambaye amekuwa katika kiwango cha juu kuliko wengine wote katika msimu huu.

Gerrard aliyeichezea Liverpool mechi 471 na kufunga mabao 111 ana kipaji, uwezo wake uko juu lakini mambo anayoyafanya msimu huu, yanaonyesha anakubalika kama kweli ni babu kiumri katika soka ni kijana tena sawa na ‘brazamen’ kabisa.


Nini asichoweza, uwezo mkubwa katika kukaba, pasi nyingi za mabao, mabao mengi ya kufunga hata kuliko washambuliaji nyota kama Robin van Persie wa Man United au Samuel Eto’o wa Chelsea. Hata ukisema mengi ni ya penalti, bado haiondoi maana ya mabao aliyofunga, yanahesabika.

Lakini Gerrard unaweza kumfananisha na bibi kizee ambaye kadiri umri unavyozidi kuongezeka, sura yake inazidi kuwa yenye mvuto zaidi na hilo linaweza kudhibitishwa na uwezo wake mkubwa uwanjani na namna ambavyo amekuwa akiichezesha timu yake.

Pamoja na kuwa mchezeshaji mzuri kwa maana ya mwanzilishi wa mashambulizi, lakini ametoa pasi 9 zilizozaa mabao yaliyofungwa na Luis Suarez, Daniel Sturridge na washambuliaji wengine wa Liverpool katika ligi hiyo ngumu zaidi duniani.

Umri wake ni mkubwa, lakini Kocha Brendan Rodgers ameonyesha kiasi gani anazidi kumuamini kwani amempa nafasi ya kuanza katika mechi 23, ameingia katika mechi tano na zilizobaki alikuwa ni mgonjwa.

Lakini ni kati ya wachezaji wa Liverpool ambao wamepiga pasi nyingi zaidi wanapokuwa uwanjani, amepiga 1,465 na kufanikiwa kufikisha sehemu sahihi pasi 1,253, amepata wastani wa asilimia 85 ambao ni kati ya ule wa juu kabisa.

Gerrard anazidi kuonyesha ni mchezaji aliyekamilika kwa kuwa pamoja na pasi bora, kufunga mabao, pasi za mabao lakini ana takwimu nzuri ya mashuti aliyopiga na yaliyolenga lango.

Ingawa ana kasi kubwa ya kuchezesha timu, lakini amepiga mashuti 32 na kati ya hayo 21 yamelenga lango msimu huu. Hii pia inaonyesha kiwango chake kipo juu.

Kuna wachezaji wengi ambao ni wageni kwenye Ligi Kuu England, lakini pia wale wenyeji na wenye umri wa chini sana kwake, lakini hawajafikia hata nusu ya takwimu ambazo amezipata msimu huu ambao Liverpool kwa mara ya kwanza ndani ya miaka zaidi ya 10, imerudi na kuwa timu inayopambana kupata taji na si kuwania nafasi ya nne au nafasi ya kucheza Europa Cup.

Kuna wakati mtangazaji mmoja wa runinga maarufu ya michezo ya Uingereza ya SkySports aliwahi kusema, Gerrard ni nahodha kweli kwa kuwa hata ukipanga kikosi cha manahodha 11 kutoka timu mbalimbali maarufu, basi bado Gerrard ataendelea kuwa nahodha, na ndicho anachoonyesha sasa.
 
Maana ni ng’ombe asiyezeeka maini, mpiganaji mwenye mapafu ya mbwa na mtu mwenye roho ya paka anayetaka kupata kinachotakiwa na hasa ubingwa wa Premiership.

MECHI:
Alizoanza 23
Alizoingia 5

PASI
Alizopiga 1465
Zilizofika  1253
Wastani 85%

KROSI 131

PASI ZA MABAO 9

MASHUTI:
Aliyopiga 32
Yaliyolenga 21
MABAO 13




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic