Kitendo kilichofanywa na wachezaji wa
Yanga kuliondoa langoni na kulitupa kwa mashabiki taulo la kipa wa Simba, Ivo
Mapunda, kimemkera kipa huyo na kufunguka wazi kuwa sababu kubwa iliyowafanya
wachezaji hao kufanya hivyo ni kutokana na kuamini imani za kishirikina.
Tukio hilo lilitokea juzi Jumamosi
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar timu hizo zilipokuwa zikiumana na matokeo kuwa sare
ya kufungana bao 1-1.
Baada ya mpira uliopigwa na Msuva
kuelekea langoni mwa Simba kuokolewa na Ivo ndipo Hamis Kiiza wa Yanga
alikimbilia golini hapo na kuliondoa taulo hilo lililokuwa likining’inia kwenye
nyavu za lango hilo na kulitupa chini kisha ndani ya nukta chache Didier
Kavumbagu naye aliliokota na kwenda kulirusha kwa mashabiki ambao nao
walilichanachana na kugawana vipandevipande.
Kocha wa makipa wa Simba, Idd Pazi,
aliinuka mara moja akitokea kwenye benchi la ufundi la timu hiyo akiwa na taulo
lingine mkononi na kulipeleka kwa kipa huyo ambaye naye akalining’niza nyavuni
kwa mara nyingine, ndipo Mrisho Ngassa alilifuata na kulitoa tena na kuibua
mtafaruku wa aina yake baina ya wachezaji wa timu hiyo lakini mwamuzi Dominic
Nyamisana alilimaliza suala hilo na kumzawadia Kavumbagu kadi ya njano.
Dakika chache baadaye wakati mpira
unaendelea, shabiki mmoja ambaye hakujulikana mara moja jina lake, aliruka uzio
uwanjani hapo na kuliiba taulo hilo kisha kuwarushia tena mashabiki wa Yanga
lakini baada ya tukio hilo, shabiki huyo alitiwa nguvuni na polisi waliokuwapo
uwanjani hapo.
Mara baada ya mpira kumalizika, Ivo
alisema: “Sijui ni kwa nini wachezaji wa Yanga waliamua kufanya hivyo, si
kitendo cha kiungwana hata kidogo kuliondoa taulo langu na kulirusha kwa
mashabiki, nafikiri walifanya hivyo wakiamini pengine lile taulo lina mambo ya
kishirikina na hili nimekuwa nikilisikia mara kwa mara kutoka kwa watu
mbalimbali kwamba lile taulo linahusishwa na imani za kishirikina kitu ambacho
hakina ukweli wowote.”
0 COMMENTS:
Post a Comment