April 19, 2014


Na Shaban Mbegu wa CHAMPIONI JUMAMOSI
USIKU wa Mei 9, 2010 ilikuwa ni siku ya furaha kwa wanachama, mashabiki na wapenzi wa timu ya Simba baada ya kupata safu mpya ya uongozi wao katika uchaguzi uliofanyika katika Bwalo la Maofisa wa Polisi lililopo Oysterbay, jijini Dar.

Katika uchaguzi huo Ismail Aden Rage alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa klabu ya Simba baada ya kushinda kwa idadi ya kura 785 dhidi ya mpinzani wake Hassan Hassanoo aliyepata kura 435.
Nafasi ya makamu mwenyekiti ilikwenda moja kwa moja kwa Godfrey Nyange Kaburu ambaye alipita bila kupingwa. 
Wengi walikuwa na imani na Alhaj Rage kutokana na historia ya kiongozi huyo katika mchezo wa soka tangu alipokuwa mchezaji wa timu hiyo, katibu wa timu hiyo na kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (Fat).
Lakini kiongozi huyo tangu alipoingia madarakani hakuna alichofanya cha maana zaidi ya kuiangamiza timu hiyo na kuiingiza katika migogoro na hasara kubwa mpaka sasa akiwa amebakiza siku kadhaa kabla ya kumaliza muda wake mwezi ujao.
Kiongozi huyu alijisahau na kuleta siasa na maneno mengi kwa timu hiyo, na kusahau kuwa kabla ya kuchaguliwa alikuwa mstari wa mbele kumbeza mzee Hassan Dalali ambaye ndiye aliyempokeza kijiti.
Rage alisahau ule msemo wa wahenga kuwa uhondo wa ngoma ni kuingia kucheza, alianza kujinasibu kwa maneno mazuri na matamu kabla ya kuingia madarakani lakini matokeo yake akaitumbukiza timu kwenye shimo.
Yafuatayo ni matukio ya uongozi wa Rage katika miaka minne aliyokaa na timu hiyo.

Uwanja wa Simba
Rage wakati anaingia madarakani alidai atajenga uwanja ndani ya siku 90, lakini muda huo ulipita na siku alipoulizwa, kama kawaida yake mzee huyo wa maneno mengi akadia kuwa kama serikali ilijenga Uwanja wa Taifa kwa miaka 50, Simba itaweza vipi kujenga kwa siku 90?

Kuuza wachezaji
Kiongozi huyu alipoingia madarakani aliingia na sera ya kuuza wachezaji na alianza na Mbwana Samatta aliyeuzwa kwa klabu ya TP Mazembe kwa dola 150,000 .
Kwa mujibu wa Rage alisema katika fedha hizo, klabu itapata dola 100,000, wakati Samatta atapata dola 50,000 kama ada ya uhamisho.
Mazembe walivutiwa na Samatta baada ya kucheza na Simba mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika na kuitoa Simba. Katika mchezo wa marudiano Samatta aliwatoka mabeki wanne wa Mazembe na kufanikiwa kumtoka kipa wa Mazembe Robert Kidiaba na kusawazisha bao 2-2 kabla ya TP Mazembe kuongeza goli la tatu.
Baada ya mchezaji huyo akafuata kiungo wa timu ya taifa ya Uganda 'The Cranes' na Simba, Patrick Ochan, ambaye pia aliuzwa kwa Mazembe.
Kama hiyo hatoshi ndani ya miaka hiyo minne ya Rage pia aliuzwa kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo Mganda Emmanuel Okwi dola kwa 300,000 kwenda klabu ya Etoile Du Sahel ya Tunisia.
Kibaya zaidi mpaka sasa wakati Rage anaelekea kuondoka katika timu hiyo  pesa za mchezaji huyo hazijalipwa na hakuna dalili za kulipwa. Kama Rage alishindwa kuzipata akiwa madarakani haitawezekana kuzipata akiwa nje ya Simba.
Mwaka 2013 ni kama vile ndiyo Rage aliamua kweli kuwafanya Simba mambumbumbu kama mwenyewe alivyowaita, aliuzwa kiajabu kiungo mahiri wa Simba, Mwinyi Kazimoto, huko Qatar. Pia Wana-Simba wakiwa bado hawajaamka usingizini Rage akamtoa bure kiraka wa timu hiyo, Shomari Kapombe, kwenda AS Cannes ya Ufaransa, kibaya zaidi mchezaji huyo amevunja mkataba na sasa kuna kila dalili atacheza Azam msimu ujao.
Zengwe la wachezaji
Katika miaka minne ya Rage aliiingiza timu hiyo mkenge kwanza kwa Mbuyu Twite ambaye alimsajili kutoka APR ya Rwanda. Mchezaji huyo alitangazwa kwa mbwembwe nyingi siku ya Simba Day na kuonyeshwa jezi yake namba 4, kumbe hakufuata utaratibu na matokeo yake Yanga wakamzidi ujanja na mpaka sasa anacheza huko.
Pia Kelvin Yondani na Mrisho Ngassa  wakati wanahusishwa na kujiunga na Yanga, Rage mara kadhaa alijinasibu kuwa hawawezi kwenda timu hiyo lakini mwisho wa siku nyota hao wakatua Jangwani.

Magarasa
Uongozi wa Rage ndiyo uliongoza kwa kusajili wachezaji magarasa ambao wengi wao walivunja mikataba, baadhi yao ni kama Daniel Akuffor, Pascal Ochieng, Gervas Kago, Komabil Keita, Salum Kinje, Kanu Biavyanga na Mussa Mude.
Kujiuzulu kwa Kaburu
Katika safari ya Rage akiwa kiongozi mkuu wa timu hiyo anamaliza muda wake bila ya uwepo wa makamu wake Godfrey Nyange ‘Kaburu’ambaye alijiuzulu Machi 2013.
Kaburu alifikia hatua ya kujiuzulu kutokana na kile alichodai kusakamwa sana na wanachama wa timu hiyo, na wakati anajiondoa kundini alikuwa safari moja na bosi wa usajili Hans Pope. Rage wakati viongozi hao wanaandika barua ya kuachia nafasi zao alikuwa nje ya nchi na aliporudi akakubali kuondoka kwa Kaburu lakini Hans Pope akapinga.
Msiba wa Mafisango
Kiungo mkabaji wa kimataifa aliyekuwa akiichezea timu ya Simba, raia wa Rwanda, Patrick Mutesa Mafisango, alifariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Chang’ombe, Dar es Salaam usiku wa kuamkia Mei 17, 2012.
Mafisango alizikwa Lemba nje kidogo ya jiji la Kinshasa DRC Congo. Atakumbukwa daima na wapenzi wa soka, lakini msiba wake haukusimamiwa inavyotakiwa. Kwanza alisafiri kiongozi mmoja pia hata mchezaji alikwenda mmoja huku pesa za rambirambi zikipigwa danadana kwa muda mrefu.
Wachezaji kuondoka
Katika miaka minne ya Rage moja ya sababu zilizoivuruga timu hiyo ni migogoro na wachezaji, wengi walifungiwa bila sababu za msingi na kupewa tuhuma, hali iliyopelekea kuondoka kwa mastaa muhimu wa timu hiyo kama Haruna Moshi, Juma Kaseja na Juma Nyoso.

Kamati kumsimamisha Rage
Novemba 19, 2013 Kamati ya Utendaji ya ya Simba ilitangaza kumsimamisha Rage kwa kile kilichotajwa ni kutokuwa na imani naye.
Wakati kamati hiyo inafikia maamuzi hayo Rage alikuwa nje ya nchi na alipotua nchini akapinga kusimamishwa kwake, baada ya vikao kadhaa vya majadiliano na hali ikatulia.
Kubishana na TFF
Baada ya kutokea hali ya kutoelewana kati yake na timu ya Kamati ya Utendaji ambayo ilimsimamisha, TFF iliingilia kati na kumtaka Rage kuitisha kikao cha dharura, lakini kiongozi huyo mara kadhaa alitumia waandishi wa habari kubishana na taasisi hiyo inayosimamia soka.
Kuteua wajumbe bila mpango
Rage katika miaka yake ya uongozi alikuwa na tabia ya kuchukua madaraka bila kushirikisha viongozi wenzake, jambo ambalo nalo lilikuwa chachu ya mvurugano, ni pale alipomteua Michael Wambura na Rahma Al Kharoos ‘Malkia wa Nyuki’.
 
WANACHAMA WAMECHARUKA BAADA YA KUWAITA MBUMBUMBU, HAPA WALITAKA KUMCHAPA RAGE HADI POLISI WALIPOINGILIA.
Kuwatusi wanachama
Rage katika mkutano mkuu maalumu uliotishwa kwa ajili ya kufanya marekebisho ya katiba Rage aliwaita ‘mbumbumbu’.
Kufuatia kauli hiyo, Rage, alilazimika kuwaomba radhi wanachama hao zaidi ya 571 waliohudhuria mkutano huyo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi, Oysterbay jijini Dar.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic