Muuaji wa bao la tatu kwenye mchezo wa kirafiki kati ya Taifa Stars na Burundi ‘Intamba Murugamba’, Yusuf Ndikumana, ana asili ya Tanzania.
Jumamosi ya wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, timu
ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ilishindwa kufurukuta baada ya kukubali
kipigo cha mabao 3-0, huku bao la tatu likifungwa kwa umbali wa mita 50 na
kiungo wa timu hiyo, Ndikumana.
Ndikumana
amesema kuwa bao alilofunga amemzawadia baba yake mzazi, Shekhe Songoro
Mustafa, ambaye ni Mtanzania anayeishi hapa nchini.
“Najisikia raha sana kufunga bao kama lile ambalo nalipeleka kwa
baba yangu Shekhe Songoro Mustafa, ambaye ni Mtanzania ila alikuja Burundi
kikazi miaka ya nyuma na kunizaa baada ya kumuoa mama yangu ambaye ni raia wa
Burundi.
“Bao lile ni la kwake kwa sababu yeye ndiye mtu aliyeniambia
nikiingia katika mchezo ule nitulie ili niweze kufunga kwani riziki huwa
zinakuja kwenye nafasi na hata nilipokuwa na mpira nilimuona kipa amesogea kwa
mbele ndipo nikaupiga na kuingia moja kwa moja wavuni,” alisema Ndikumana.
Ndikumana anacheza katika Klabu ya Lydia Ludic Burundi Academie
inayoongoza ligi ya nchi hiyo huku ikibakiwa na michezo nane kumaliza ligi
hiyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment