MWOMBEKI AKIPAMBANA NA MABEKI WA PRISONS |
Mshambuliaji wa Simba, Betram Mwombeki, amesema kwamba yupo tayari
kuvunja mkataba na klabu hiyo endapo ataendelea kusota benchi na kukosa amani
kwenye kikosi hicho msimu ujao.
Mwombeki aliyesajiliwa na Simba iliyokuwa chini ya Abdallah
Kibadeni msimu uliopita, alikuwa shujaa wa timu hiyo kwenye mechi kadhaa hasa
ile dhidi ya watani wao, Yanga, pale alipofunga bao na kuisaidia timu hiyo
kutoka nyuma na kuilazimisha Yanga sare ya mabao 3-3 kwenye ligi kuu msimu
uliopita.
Lakini baada ya muda mfupi mambo yalimbadilikia straika huyo na
kuanza kusugua benchi huku mara kwa mara akikosekana kwenye mazoezi ya timu
hiyo baada ya kutua kwa utawala wa Mcroatia, Zdravko Logarusic.
Mwombeki alisema huwa hafurahii
maisha aliyonayo Simba kwa sasa, hivyo endapo msimu mpya utaanza na mambo
yatakuwa ni yaleyale, basi atakuwa hana budi kuachana na timu hiyo na kuangalia
maisha mengine.
Mwombeki amebakiza mkataba wa mwaka mmoja klabuni hapo unaoisha
mwishoni mwa msimu wa 2014/15.
“Haina haja ya kukuelezea sana kwamba nilikuwa naishi maisha gani
Simba, kila mtu aliyekuwa anafuatilia soka alikuwa anaona kilichokuwa
kinaendelea, lakini kama itatokea mambo haya yataendelea msimu ujao basi
nitavunja mkataba na kuangalia mambo yangu mengine.
“Naweza nikatafuta timu nikacheza au nikaangalia maisha yangu
mengine na nikatulia kwanza kuhusu soka.
“Siwezi kusema kwamba Loga ndiyo chanzo kwa sababu yeye amekuja na
mfumo wake mpya na kila kocha anakuwa na mipangilio yake katika timu, lakini
kuna vitu vingi muda mwingine huwa vinaendelea na mimi huwa siridhishwi navyo.
“Ishu kubwa ni kwamba mimi nacheza mpira, sasa kama mtu unacheza
soka ni lazima watu wakuone uwanjani na si kukaa benchi tu, hii inakuwa haipendezi,
soka ni mchezo wa kuonekana, sasa kama mtu unakuwa hupewi nafasi ina faida gani
sasa?” alihoji Mwombeki.
0 COMMENTS:
Post a Comment