Na Saleh
Ally
MWISHO wa
Rio Ferdinand katika kikosi cha Manchester United, haujaenda kama ambavyo wengi
walitarajia.
Rio
hataonekana tena kwenye kikosi cha United na msimu huu mbaya kwa kikosi hicho,
umekuwa wa mwisho kwake.
Kizazi kingine cha Alex Ferguson kinaondoka kwenye kikosi hicho lakini uondokaji wake unaonekana si mzuri kwa kuwa wengi walitarajia kuwa Rio alipaswa kuagwa kwa mashamsham ikiwezekana ndani ya Uwanja wa Old Trafford, lakini haikuwa hivyo.
Shukrani
za Manchester United kwa Rio zimepitia kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter
kwenye akaunti ya klabu hiyo.
Maneno
haya yameandikwa: “"#mufc inapenda kumshukuru Rio
Ferdinand kwa uhudumu wake wa muda mrefu na wenye mafanikio na tunamtakia
mafanikio zaidi katika maisha yake baadaye.”
Maneno hayo ni ya kiungwana, lakini
kwa kuchimba zaidi yanaonyesha mpira hauna shukrani, hauna adabu na si Tanzania
pekee, bali England na duniani kote.
Miaka 12 ikiwemo 11 ya mafanikio
katika klabu hiyo tokea alipojiunga nayo akitokea Leeds kwa kitita cha pauni
milioni 30 (zaidi ya Sh bilioni 78) na kuweka rekodi ya kuwa beki na mchezaji
ghali zaidi katika kipindi hicho siyo michache.
Katika kitabu cha mwisho kuhusu
maisha yake, Ferguson amebainisha kuwa Manchester United imekuwa ikifanya
vizuri zaidi kila inapokuwa na mabeki wa kati wa uhakika akawatolea mfano Garry
Pallister na Steve Bruce na baadaye kipindi cha akina Rio na mwenzake Nemanja
Vidic.
Mapenzi makubwa ya Rio kwa timu hiyo
yako wazi, alipambana kwa kila namna hadi ilipofikia “akili inataka, mwili
hauna uwezo.”
Ndiyo maana akaomba kubaki Old
Trafford kwa msimu mmoja zaidi, lakini imeshindikana, klabu imemueleza katika
hatua za mwisho kwamba haitaweza kuendelea naye huku yeye akiwa na uhakika
angepata nafasi.
Kutokana na hali hiyo, inaonekana Rio
hakutegemea, hali hiyo ikamchanganya na haraka akaandika kwenye mtandao wake
hivi: “Nimekuwa na wakati mgumu wa kutafakari wakati wa miezi michache
iliyopita kuhusiana na miaka 12 katika klabu hii bora duniani, lakini mwisho
nimeamua kuondoka.
“Nilijiunga na Manchester United kwa
matumaini ya kushinda vikombe, najisikia furaha nimekuwa na mafanikio makubwa,
kuna mengi ya kukumbuka, mfano tulivyotwaa ubingwa wa Ulaya kule Moscow.
“Inawezekana sikupata nafasi ya
kuwaaga mashabiki kama ambavyo nilitaka, lakini sasa najisikia niko vizuri
zaidi na tayari kwa lolote kutokana na maisha yatakavyokuwa.”
Maneno ya Rio yana maana kubwa,
anaonyesha kiasi gani ambavyo hakupewa nafasi ya kuwaaga mashabiki, lakini
anasisitiza yuko fiti, maana yake klabu ndiyo haikutaka aendelee.
Kutoendelea linaweza kuwa jambo la
msingi kwa kuwa miaka 35 huenda inatosha hasa kwa beki na timu kama Man United
ikizingatiwa alikuwa majeruhi mfululizo. Lakini aina yake ya kuondoka, si
sahihi.
Tayari Man United imeanza juhudi za
kumnasa beki ngangari mwenye miaka 18 tu, huyu ni Luke Shaw ambaye wametaka
kutoa pauni milioni 27 lakini Southampton wamesema wanataka 30.
Rio anaondoka United akiwa beki
aliyecheza kwa mafanikio makubwa zaidi katika kipindi cha Ferguson huku misimu
miwili akichukua namba moja kwa mchezaji aliyepiga pasi nyingi kwa msimu baada
ya Fergie kuanzisha mfumo wa timu kuchezeshwa na mabeki wa kati.
Hadi msimu uliopita unaisha, Rio
alicheza mechi 14 tu kwa United lakini ndiye beki mwenye uwezo mkubwa zaidi wa
kupiga pasi zinazofika kuliko mwingine. Ubora wa pasi zake ni asilimia 89 ambao
ni wa juu kuliko hata viungo wengi nyota katika ligi hiyo.
Tottenham imeandaa mechi maalum ya
kumuaga beki wake wa kati Ledley King ambaye ameichezea mechi 268 katika
kipindi cha miaka 13, wakati katika miaka 12, Rio ameitumikia United katika
mechi 312. Hii inaonyesha, anastahili kuagwa kwa heshima, apewe heshima yake.
Mwache Rio aende zake, lakini
anaondoka bila ya kupata heshima yake. Funzo kwa wengine England, lakini hata
hapa nyumbani Tanzania. Rio ni jembe kweli.
TAKWIMU:
MISIMU
MIAKA
MECHI
MABAO
2002-2014
12
312
7
0 COMMENTS:
Post a Comment