June 28, 2014


AVEVA 'EEA'

KESHO ndiyo mwisho wa ubishi kwa wanachama wa klabu ya Simba ambao wameusubiri kwa hamu kubwa uchaguzi wa viongozi wao.
Aveva anafunga rasmi kampeni zake leo kwenye hoteli moja kubwa jijini Dar es Salaam na mambo yanavyokwenda, Wanasimba watamchagua yeye kuwa rais wa kwanza wa Simba tokea ianzishwe.

Evans Elieza Aveva ‘Eea’ ni kati ya wanaowania nafasi ya urais akiwa na mgombea mwingine Andrew Tupa. Lakini inaonekana Aveva ndiye anayepewa nafasi zaidi.
Tayari ameanza kampeni zake kwa kupita sehemu mbalimbali ikiwemo kibaha na kwingineko. Lakini akasisitiza kuwa mengi atamwaga wakati atakapopewa nafasi kesho mbele ya wanachama.
Aveva ambaye si mzungumzaji sana anasema amejikita kwenye vitendo na anaamini Wanasimba wengi wanaijua kazi yake ingawa amesisitiza kuna mambo matano yanaweza kuwa sababu ya yeye kupewa urais wa Simba.

1
Usajili:
Nimekuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili, lakini nimekuwa mjumbe wa kamati hiyo mara nyingi hivyo ninajua nini kifanyike wakati wa usajili.
Suala hilo litakuwa chini ya kamati ya usajili ambayo ina watu imara na wazoefu, lakini bado ninaweza kuwa msaada kwao kwa kuwa ninajua njia za kupita.
Kipindi ambacho Simba ilikuwa imara, ndiyo nilikuwa nikiongoza kamati au kati ya usajili. Sasa ushindani utakuwa umeongezeka, lakini hakuna cha kuizuia Simba kufanya inachotaka, ushindani ni sehemu ya changamoto.

2
Uongozi:
Nina uzoefu, nimewahi kukaimu hadi nafasi za juu kabisa Simba. Lakini kuongoza kamati ya usajili, kuongoza Friends of Simba (FOS) ambayo imekuwa ni injini, kwangu ni uzoefu tosha.
Sina hofu hata kidogo na kama nikiingia madarakani, huenda nikawa kiongozi mzoefu zaidi kuliko wa klabu nyingine zote. Hivyo siwezi kuwa na hofu na jambo lolote pia ninajua kutakuwa na msaada mkubwa kutoka kwa Wanasimba wanaotaka maendeleo, siwezi kufanya kila jambo la mafanikio peke yangu.

3
Umoja:
Nimekuwa nikisisitiza sana suala la umoja, nataka Simba moja yenye watu wenye lengo moja, kuendelea. Ninaamini hata hizi tofauti ziko wakati huu wa uchaguzi, lakini litakuwa suala la msingi baada ya hapo tuungane.
Sioni kama itakuwa sahihi kujenga makundi, tukikubali hivyo ni sawa na kukubali kurudi nyuma wenyewe wakati tukijua dhambi ya kutengana ni kubwa na mwisho wake ni kutusambaratisha, nisingependa itokee.

4
Uzoefu:
Wakati naanzisha kundi la Friends of Simba mwaka 1999, niliona kuna tatizo na Simba ilikuwa katika hali ngumu kifedha. Nikatafuta watu ambao wangekuwa tayari kuichangia kwa kuwa wakati ule usipokuwa mwanachama ilikuwa vigumu kuingia na kutoa michango.
Kuanzia hapo, nimekutana na watu wengi, nimeshirikiana na viongozi wengi waliopita wa Simba. Hivyo uzoefu wangu si wa kuhoji tena na ninajua Simba imepita wapi tokea mwaka 1999.
Lengo ni kuleta mafanikio, hivyo mbinu ziko nyingi. Kwa kushirikiana na viongozi, marafiki na wanachama, lazima kutakuwa na mabadiliko makubwa.

5
Yanga:
Najua kila mtu angefurahia kuona ule ufalme wa Simba kama kuinyanyasa Yanga kwa miaka saba mfululizo unarejea. Hakuna shaka hilo linawezekana ingawa katika Simba ya kisasa watani wetu hao wanaweza kuwa sehemu.
Kuifunga Yanga ni jambo zuri, lakini kuwa na Simba ya kimataifa inayofanya vizuri kimataifa ni jambo zuri zaidi. Usisahau Simba ni timu yenye rekodi za juu zaidi katika michuano ya kimataifa nchini.
Hilo lazima liendelezwe na linawezekana, lakini halitakuwa linafanikiwa kilahisi badala yake kiongozi imara kama mimi, ushirikiano kutoka kwa viongozi wengine bora, wanachama na mashabiki, basi Simba itakuwa bora na isiyokamatika.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic