June 9, 2014




SIKU moja tu baada ya kupata taarifa kwamba uongozi wa klabu ya Coastal Union ya Tanga imetangaza harambee ya wanachama na mashabiki wake kuichangia, nikapata taarifa nyingine tofauti.
Taarifa za safari hii ni kwamba kampuni ya Bin Slum Tyres ilikuwa iko katika hatua za mwisho za kuingia mkataba na Mbeya City.
Mkataba huo wa miaka miwili utagharibu hadi Sh milioni 360 kwa miaka miwili, haraka nikazigawanya fedha hizo na nikapata jibu kuwa ni shilingi milioni 180 kila mwaka wagonga nyundo hao wa jiji la Mbeya watakuwa wanapata kutoka kwa Bin Slum Tyres.
Kwanza niliona ni jambo zuri, mfano wa kuigwa na itakuwa ni jambo jema kuanza kuwapongeza Mbeya City na baada ya hapo kampuni hiyo ya Bin Slum Tyres, nitaeleza kwa nini.
Ubora wa Mbeya City, kufanya mambo yao kwa mpangilio ndiyo kimekuwa kitu kilichochangia kuwavuta Bin Slum Tyres wakubali kuwadhamini kwa kutoa mamilioni ya fedha. Udhamini huo si kiduchu kwao, unazidi hata ule wa Azam TV ambayo hutoa milioni 100 kwa kila timu.
Pili kuwapongeza Bin Slum Tyres kwa kuona ubora wa Mbeya City, kwamba wanajituma na wanafanya mambo yao kwa mpangilio vilivyo, wakaaua kuutumia mpira kujitangaza. Hilo ni jambo la faraja kwa wapenda soka kwa kuwa wadau tunaotaka maendeleo tunaka wenye fedha zao wajitokeze na kuusaidia mpira.
Hivyo ni jambo jema kuwapongeza Bin Slum Tyres na Mbeya City kwa jambo hilo zuri walilolifanya, pia litakuwa ni mfano mzuri kwa wengine wanaotaka kujifunza kwamba soka inawahitaji wadhamini, nao wanaiihitaji pia, hivyo wengine zaidi wajitokeze kufuata mfano huo wa Bin Slum.
Wakati tunawavuta wengine, pia kuna jambo la kujadili na kama unakumbuka kulikuwa na mgogoro uliojaa mambo yasiyokuwa na maana, malumbano ambayo yalionyesha hayakuwa na tija sana kwa ajili ya klabu na badala yake mtu mmoja kumchukia mwingine na wakasahau klabu inataka nini.
Bin Slum aliyeamua kuidhamini Mbeya City, alikuwa akijitolea Coastal Union na alisema ametoa zaidi ya Sh milioni 300. Lakini mwisho akaambulia dharau na maneno mengi kutoka kwa viongozi wa klabu.
Viongozi nao wakawa na mambo mengi, ikiwemo kuhakikisha wanazuia wanachama wapya kuingia kwa hofu ya vyeo vyao kuchukuliwa. Hata sasa wanaweza hata aondoke Bin Slum, Coastal Union wataendelea kuwepo. Watakuwa sahihi, kwani hata wakiondoka wao, bado itaendelea kuwepo, kitu kikubwa ni maendeleo husika katika wakati mwafaka.
Sasa wanapitisha bakuli, wanataka mchango wa fedha kutoka kwa wanachama na mashabiki, kitu ambacho hatukuwahi kukisikia wakati wa Bin Slum akifanya nao kazi.
Inawezekana aliwabana sana katika kuchota fedha? Au kwa fedha za harambee, ni lahisi sana kwa viongozi kujichotea na kufanya wanavyotaka bila ya kuhojiwa na yoyote kuliko zile za mdhamini anayefuatilia kuhusiana na fedha zake zinavyotumika kama ilivyokuwa kwa Bin Slum? Haya ni maswali tu, majibu tutapata kadiri siku zinavyosonga mbele.
Maswali yatajibiwa na muda, lakini ukweli katika klabu karibu zote zinazoongozwa kwa mfumo wa wanachama kuna matatizo makubwa na viongozi wengi wanataka ziende kwa mfumo wa kizamani.
Wasiulizwe, wakiharibu waachwe, wasishauriwe kwa kuwa wanajua sana na mwisho kigezo chao ni kwa kuwa wao wamechaguliwa na wanachama. Matatizo mengi yanaanzia hapo na mwisho zinakwama na kubaki na ukubwa wa jina.
Hakuna timu au klabu inaweza kupata mafanikio bila ya kuwa na wadhamini wanaoisapoti. Mambo yanabadilika, fedha za mapato ya milangoni hazitoshi kuendesha klabu katika kipindi hiki, badilikeni eh!



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic