VITA kubwa kwa sasa inayoendelea ndani ya Ligi Kuu England ni kujua nani atakuwa bingwa kwa msimu wa 2021/22 kutokana na kila timu kuonekana kuwa imara jambo linalofanya hali kuwa ya moto kila mahali.
Timu nne zinapewa chapuo ya kuweza kusepa na taji hilo ambalo kwa sasa lipo mikononi mwa Manchester City inayonolewa na Kocha Mkuu, Pep Guardiola huku nyingine ikiwa ni Liverpool inayonolewa na Jurgen Klopp, Manchester United ya Ole Gunnar Solskjaer pamoja na Chelsea ya Thomas Tuchel.
Ngoma ni nzito kutokana na mwendo ambao wameanza nao vigogo hao ambapo Liverpool yenye Mohamed Salah raia wa Misri na Sadio Mane raia wa Senegal kutoka barani Afrika wanaongoza kwa takwimu za mabao wakiwa wametupia 17 inafuatiwa na Chelsea yenye Romelu Lukaku ikiwa na mabao 15 huku Manchester City yenye Jack Grealish ikiwa imetupia mabao 14 sawa na Manchester United yenye Cristiano Ronaldo.
Ukigusa upande wa pasi ni Manchester City hawa ni namba moja wakiwa wamepiga jumla ya pasi 4,275, Manchester United wanafuata wakiwa wamepiga jumla ya pasi 3,871 kisha Liverpool ipo namba tatu ikiwa imepiga jumla ya pasi 3,810 na pia inaongoza upande wa mashuti ikiwa imepiga mashuti 147, Manchester United mashuti 120 na City mashuti 127.
0 COMMENTS:
Post a Comment