Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Simba iliyo chini ya
Mwenyekiti, Dokta Damas Ndumbaro, imelitupia suala la aliyekuwa mgombea wa
nafasi ya urais, Michael Wambura, katika Kamati ya Utendaji kujua kama
ataruhusiwa kupiga kura ama la.
Awali Wambura aliondolewa katika kinyang’anyiro hicho
kufuatia kamati hiyo kubaini siyo mwanachama halali kutokana na kusimamishwa
mwaka 2010, ikiwa ni pamoja na kuipeleka klabu hiyo mahakamani kesi ambayo
alishinda baada ya kukata rufaa katika kamati ya rufani ya TFF, hivyo kutaka
kujua uhalali wake katika kupiga kura.
Akizungumza na Championi
Jumatano, Ndumbaro alieleza kuwa hatma ya kuruhusiwa ama kutoruhusiwa
kupiga kura kwa Wambura ipo mikononi mwa Kamati ya Utendaji ambayo ndiyo
iliyotoa maamuzi ya awali ya kumzuia mwanachama huyo, hivyo wanasubiria taarifa
kutoka katika kamati hiyo ili waweze kutoa maamuzi juu ya suala hilo.
“Kamati ambayo ilimzuia Wambura kutopiga kura mwaka 2010
ilikuwa ni hii kutokana na kupata barua kutoka katika Kamati ya Utendaji hivyo
tulimzuia kwa kutoingia katika ukumbi wa uchaguzi.
“Ni kweli alishinda rufaa yake ya awali lakini kuhusu
kumruhusu kupiga kura Kamati ya Utendaji ndiyo inayotakiwa kutoa maamuzi na si
sisi, hivyo tunasubiri barua kutoka kwao kuona kama watamruhusu ama la.
“Tutawasiliana na Kamati ya Utendaji ili iweze kutupa hadhi
yake kwa sasa kuona kama anaruhusiwa kupiga kura,” alisema Ndumbaro ambaye ni
mmoja wa wanasheria maarufu nchini.
SOURCE; CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment