USHINDI wa
rufaa ya Michael Richard Wambura umeonekana kuwashangaza kwa kuwa maswali sasa
yamehamia katika suala la sheria kama inawezekana watu kupiga kura katika jambo
linalohusu vifungu vya kisheria!
Maswali
hayo yanaweza yakawa muhimu kwa
kuwa watu wanataka kujifunza, nafasi wanayo kwa kuwa wanasheria ni wengi,
lahisi kuuliza na jibu likapatikana kama jambo lilikuwa sahihi au la!
Lakini
inawezekana bado jambo hilo halitakuwa ndiyo la muhimu zaidi kuliko yote kwa
Wanasimba ambao wiki mbili na ushee tayari watakuwa kwenye viti vyao kufanya
uchaguzi wa Rais mpya wa Simba.
Mungu pekee
ndiye anayejua nani atakuwa rais wa Simba, Evans Aveva, Wambura au……. Lakini
kitu cha mwisho kabisa ni suala la umakini na umuhimu wa uongozi, kwamba
atakayechukua na timu yake wataifanyia nini Simba.
Simba
haistahili matesho ya miaka mingine minne tena kama ilivyokuwa katika uongozi
uliopita wa Ismail Aden Rage ambaye alisema mengi bila ya kutekeleza. Mwisho
akaondoka na kuacha makovu mengi, ahadi nyingi ambazo hakuzitekeleza pia!
Kipindi
hiki, unaweza mambo sasa safi, Wambura amerudishwa na wanachama hasa wale ambao
walikuwa wakitaka hata kanuni zikiukwe, arudishwe ili agombee na wanachama
ndiyo wawe waamuzi wa mwisho, sasa wana nafasi ya kumchagua kiongozi
wanayemtaka.
Nafasi si
kila kitu, kuchagua tu bila ya kutakafakari pia ni ujuha! Lazima kila
Mwanasimba awe makini, atafakari kabla ya kuandika kwenye karatasi yake na kitu
kizuri, Aveva na Wambura hakuna ambaye atakuwa mgeni kwao.
Kikubwa wawe
huru, wasishinikizwe na mtu au kwa kuwa Wambura amerejea baada ya kurudishwa na
kamati ya rufaa ya TFF, basi ndiyo aonekane ni shujaa, la hadha! Kikubwa
kinachotakiwa wamuangalie na wapate uhakika, kuwa kweli ataisaidia Simba
ilipokwama sasa, inaishi katika maisha si ya hadhi yake, hali kadhalika kwa
Aveva na….
Kwenye
kipindi hiki cha uchaguzi, kila utakachoandika ni lawama, watu wengi sana
hawawezi kujibu hoja na msingi wa wanachokiona ni kulaumu. Mimi sibabaiki hata
kidogo, ndiyo maana nilisema mabaya ya uongozi uliopita bila ya woga, leo kila
kitu kimeonekana.
Simba
ikidorora mpira wa Tanzania hauwezi kwenda kwa kasi, hakuna anayeweza kubisha
kuwa nguvu ya Simba na watani wake Yanga ni kubwa. Ndiyo maana Azam FC ina kila
kitu lakini baso haifikii hata robo ya nguvu ya wakongwe hao.
Hivyo,
kuweni wakweli, acheni upambe, achaneni na kulalamika kwa kila jambo, badala
yake chagueni bila ya ushabiki, shinikizo wala vijisenti vya nauli. Ihurumieni
Simba, onyesheni kweli mnapenda maendeleo ya mpira hapa nyumbani. Kila la
kheri.
0 COMMENTS:
Post a Comment