Na Saleh Ally
NINGELIJADILI suala la umasikini wa mabondia wa
Tanzania katika kipindi cha wiki tatu zilizopita, mngeweza kusema mimi ni mtu
mwenye hila sana, lakini bado nisingekuwa na sababu ya kuhofia.
Lakini sasa naona ni wakati mwafaka kabisa wa
kujadili suala la mabondia wa Tanzania kuendelea kuwa masikini, wasio na
uhakika hata na mlo wa siku tu licha ya kushikilia mikanda mikubwa au kucheza
mapambano makubwa.
Kwa
mujibu wa jarida la Forbes la Marekani, mchezo wa ngumi za kulipwa ndiyo
unaolipa kuliko mwingine yoyote duniani kuanzia mwaka jana.
Mkali
wa kurusha makonde duniani, Floyd Mayweather sasa ndiye bondia anayelipwa fedha
nyingi zaidi kuliko mwingine yoyote, akifuatiwa na mwanasoka Cristiano Ronaldo
wa Real Madrid na LeBron James anayekipiga katika timu ya kikapu ya Miami Heat
ndani ya NBA, anashika nafasi ya tatu.
Kwa
mwaka jana, Mayweather ambaye sasa ameikamata dunia alilipwa kitita cha dola
milioni 105, Ronaldo akafuatia dola milioni 80 n LeBron akachukua ddola milioni
72.3.
Nafasi ya nne ni Lionel Messi wa Barcelona aliyechukua dola milioni
64.7, halafu Kobe Bryant wa LA Lakers anafunga 5 Bora kwa kuchukua dola milioni
64.5.
Ukiangalia vizuri kwenye 5 Bora hiyo utaona wanamichezo waliopo ni ngumi
(mmoja), soka (wawili) na kikapu (wawili). Pamoja na wingi wa idadi kwa michezo
mingine, lakini anayelipwa zaidi ni mwanamasumbwi, hakuna ubishi ndiyo mchezo
ulioshika dunia kwa sasa.
Hakuna
anayeweza kukataa kuwa hapa nyumbani kuna wachezaji wenye uwezo mkubwa katika
mchezo wa ngumi, wapo na wengine wamepita, lakini maisha yao yako vipi.
Kama
utasema mchezo wa ngumi haufai, basi vipi Mayweather amefikia hapo alipo, hata
kama ni Marekani. Vipi wanamasumbwi wa hapa nyumbani wasiwe angalau na uwezo wa
maisha mazuri, tatizo ni nini? Wao au watu wengine?
Kote
kuna tatizo, ndiyo maana unaona pamoja na umahiri wa Rashid Matumla na ndugu
zake ambao sasa wameangukia kwenye matatizo mengine, utagundua hakuna msingi
mzuri katika mchezo huo.
Msingi
uliopo ni ule wa watu wachache kufaidika kupitia mchezo huo na kuendelea
kuwatafuna mabondia ambao wanakuwa wanabaki na majina yao makubwa, lakini
wasiokuwa na chochote mfukoni inapofikia wakati wa kustaafu!
Maisha
ya Matumla kwa sasa, si sahihi! Anaishi katika kundi la watu wasio na uhakika
na kesho kimaisha. Ni maisha magumu lakini wako walifaidika na fedha zake na
sasa wanaendesha maisha mazuri kabisa.
Ndiko
anakokwenda Francis Cheka, Karama Nyilawila na wengine ambao vipaji vyao
vilipaswa viwalipe vilivyo kwa sasa na wangeachana na kazi ya ukondakta, uuzaji
chupa na makopo na hasa ukabaji, maana inaelezwa ni kazi ya mabondia wengi hapa
nyumbani wakiwemo wengine ambao ni maarufu!
Nani
anawasaidia mabondia, mameneja walio nao ni wa aina gani, uwezo wao ukoje?
Wanachotaka kufanya ni kwa ajili ya nini, kumsaidia bondia na wao kupata
angalau kidogo au wao kupata kingi na bondia apate angalau?
Kwa
promota ni nani, je, anaijua thamani ya mchezo wa ngumi au anaona mabondia ni
watu ‘ize’ tu, hivyo anawachukulia ‘poa’ na anaweza akafanya lolote kwa kuwa
anaamini ni watu njaa. Na kama wana njaa halafu anaendelea kuwanyoya,
kinachofuatia nini? Jibu ni kifo.
Lakini
kama kuna mabondia makini, wanahitaji mameneja, wako tayari kuwasikiliza na wao
wanaweza kuwa makini na waenda kwa misingi sahihi bila ya kuelwa sifa kama
ambavyo tumekuwa tukiona kwa watu wengi maarufu?
Hali
halisi inaonyesha kuna tatizo kubwa kwenye pande tatu, yaani mameneja wa
mabondia, mapromota na mabondia wenyewe.
Lakini
kwa kuwa wote ni wadau wa mchezo huo, lazima wakubali huu ndiyo wakati wa
kuamka, waujenge mchezo huo halafu ikiwezekana wakubali wote kula kidogokidogo,
maana yangu wagawane katika hali kila mmoja ataweza kufaidika na mchezo
ukaendelea kufanya vizuri kwa heshima na mafanikio ili uzidi kukuwa zaidi na
kuwaingizia zaidi.
Kuunyonya
mguu unaokubeba ni kujizuia kutembea kwa mwendo mzuri uliouzoea. Ikifikia hapo,
wengi watakupita kama ilivyo sasa.
Maana
wakati mchezo wa bondia unashika namba moja kwa malipo duniani, mabondia wa Tanzania
wenye majina makubwa na vipaji vya juu, wanaendelea kubaki na majina makubwa
juu, lakini wakiishi katika maisha magumu, mabaya wasiyostahili.
Shikamaneni,
jikomboeni na muamini mchezo wa ngumi una nguvu sana. Maana hata hapa nyumbani
kila mmoja anajua unashika nafasi ya pili kwa umaarufu baada ya soka.
Sasa
vipi wanasoka angalau wanaweza kuishi maisha mazuri halafu wanamasumbwi
wanabaki kama kichekesho. Ukimaliza kusoma makala haya, kama wewe ni
mwanamasumbwi au mdau wa mchezo huo, tafadhari rudia mara moja, weak gazeti
chini, chagua mkono shavuni au kichwani, halafu tafakari udhaifu wako uko wapi,
halafu rekebisha, tukikutana, utanipa jibu, ila usitumie muda mwingi kulaumu!
|
Total
|
Salary
|
Endorsements
|
Sport
|
Floyd Mayweather
|
$105m
|
$105m
|
$0m
|
Boxing
|
Cristiano Ronaldo
|
$80m
|
$52m
|
$28m
|
Football
|
LeBron James
|
$72.3m
|
$19.3m
|
$53m
|
Basketball
|
Lionel Messi
|
$64.7m
|
$41.7m
|
$23m
|
Football
|
Kobe Bryant
|
$61.5m
|
$30.5m
|
$31m
|
Basketball
|
Tiger Woods
|
$61.2m
|
$6.2m
|
$55m
|
Golf
|
Roger Federer
|
$56.2m
|
$4.2m
|
$52m
|
Tennis
|
Phil Mickelson
|
$53.2m
|
$5.2m
|
$48m
|
Golf
|
Rafael Nadal
|
$44.5m
|
$14.5
|
$30m
|
Tennis
|
Matt Ryan
|
$43.8m
|
$42m
|
$1.8m
|
American
Football
|
0 COMMENTS:
Post a Comment