UZI HUO WA WAZEE WA STAND UNITED PALE SHINYANGA |
Kampuni ya Bin Slum Tyres kupitia
matairi yake ya Double Star jana imeendelea kuonyesha kujali na kuthamini
mpira wa Tanzania baada ya kuingia mkataba wa kuidhamini Stand United ya
Shinyanga.
TUKIO LA KUSAINI MKATABA |
Baada ya mkataba huo, mlezi wa
Stand United ambaye ni mbunge wa Shinyanga, Steven Masele naye akahamasika na
kutoa basi aina ya Toyota Coaster lenye thamani ya Sh milioni 45.
Yote haya ni mambo mazuri sana
kisoka katika mkoa wa Shinyanga na kanda ya Ziwa kwa ujumla kwa kuwa ni sehemu
yenye vipaji lundo lakini imekuwa ikisonga kwa mwendo wa kinyonga.
Masele pia safi ingawa ni
mwanasiasa lakini ni vizuri kwa kuwa ametoa kwenye mpira badala ya wanasiasa
wengi ambao wamekuwa wakijifaidisha tu na soka bila ya kufanya lolote.
Lakini kama ni hongera au pongezi
kubwa inapaswa kwenda kwa Bin Slum Tyres ambaye anaonekana kuwa na jicho la
mwewe au tai.
Lina uwezo mkubwa wa kuona mbali,
lakini pia ni ujasiri mkubwa uliochanganyika na mapenzi kwa mpira wa Tanzania
hata kama itakuwa ni suala la kibishara.
Jiulize makampuni mangapi tena yale ya watu binafsi kama Bin Slum yalivyo na uoga wa kuingia kudhamini mpira wa Tanzania hata kama yanajua kuna faida.
Uoga wa makampuni hayo unataokana na kutokuwa na uhakika wa mambo, kila mtu anajua mpira wa Kitanzania, mambo mengi hayana uhakika.
Tayari kampuni hiyo imeingia
mkataba wa zaidi ya Sh milioni 350 na Mbeya City, huu ni wa miaka mitatu.
Sasa na Stand United kwa Sh
milioni 50 kwa mwaka na inawezekana wako wanaweza kuona ni mdogo sana.
Lakini jiulize mdhamini gani
anaweza kufanya hivyo kwa timu ambayo ndiyo inapanda daraja bila ya kujua
mwenendo wake?
Bin Slum Tyres imejaribu,
imejiamini na imeipa nguvu Stand United, yenyewe ndiyo ina kazi ya kuionyesha
kampuni hiyo kuwa haikukosea na baada ya msimu ujao iongeze dau na kusaini
mkataba mwingine mzuri zaidi.
Biashara na timu za soka bado
inaweza kuwa patapotea hapa nchini, lakini Bin Slum Tyres imekuwa na ujasiri wa
kuingia na kujaribu kitu ambacho kimeyashinda makampuni mengi sana.
Kwangu nasema bravo Bin Slum Tyres,
kabla ya kuanza kwa msimu ujao mmekuwa mfano wa kuigwa na kuna kila sababu ya
makampuni mengine kuiga.
Lakini kwa wadau wa soka pia wanapaswa
kuwa na mfumo mzuri wa kuendelea kuwabakiza wale walio tayari kuendelea
kusaidia mpira.
Binafsi kama nikitaka betri au
matairi ya gari langu, basi kwanza nitaanza na Bin Slum Tyres kwa kuwa wao
wanaudhamini mchezo tunaoujali, tunaoutaka na ndiyo furaha yetu.
Kununua bidhaa zao ni kuwapa
faida, ndiyo. Lakini wakipata faida, maana yake watajua mpira umewasaidia
kupata faida, hivyo hawataondoka.
0 COMMENTS:
Post a Comment