Na Saleh
Ally
KOCHA Mkuu
wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Mart Nooij ambaye ni mpya, tayari ana
rekodi unayoweza kusema ni nzuri kwa kocha wa aina yoyote ambaye ndiyo
amekabidhiwa timu.
Nooij
ameingoza Taifa Stars katika mechi nne, mbili zikiwa za mashindano na
zilizobaki ni za kirafiki dhidi ya timu moja ya Malawi.
Katika
mechi ya kwanza ya kirafiki dhidi ya Malawi, matokeo yalikuwa suluhu na timu
hizo ziliporudiana jijini Dar es Salaam, Stars ikakishinda kikosi hicho cha The
Flames kwa bao 1-0.
Kwa upande
wa mechi za kimashindano, pia ni mbili dhidi ya timu moja. Stars iliivaa
Zimbabwe katika mechi ya kuwania kucheza hatua ya makundi ili ipate nafasi ya
kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika nchini Morocco, mwakani.
Mechi ya
kwanza dhidi ya Zimbabwe, Stars ikashinda kwa bao 1-0 jijini Dar es Salaam,
baada ya hapo ikafunga safari kwenda Harare, Zimbabwe ambapo ilitoka sare ya
mabao 2-2 huku wenyeji wakilazimika kusawazisha.
Stars
imesonga mbele, sasa inakutana na timu ya zamani ya Nooij, hiyo ni Msumbiji au
Mambas na ni mechi ambayo itatoa majibu kama Taifa Stars itakwenda katika hatua
za makundi au la.
Kwa wenye
kumbukumbu, mara ya mwisho, Msumbiji ndiyo iliyoing’oa Stars katika
kinyang’anyiro cha kuwania kucheza Kombe la Mataifa Afrika. Sasa inakutana tena
na timu hiyo na haitakuwa lelemama.
Nooij
ameonyesha ana uwezo, kikosi chake hata kama hakikucheza vizuri nyumbani dhidi
ya Zimbabwe, kimekuwa na uhai na angalau kuna matumaini katika hatua ya kwanza.
Hakuna ubishi
kama kocha huyo atakwama, basi ajue Watanzania na wadau hawatakaa kimya na kama
kawaida, atavurumishiwa madongo na ikiwezekana atatupiwa virago aende zake.
Lakini kwa
kuwa ameanza kuonyesha njia ya matumaini, basi kuna jambo la kufanya mapema ili
asiingie kwenye njia ya kuharibu, si nyingine zaidi ya kumsaidia ili afanye
vizuri.
Kuna wadau
wengi wanaohusika na timu ya taifa, ingawa huduma za timu hiyo ni chini ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lakini ni timu ya Watanzania, wenye mali ni
mimi na wewe.
Hivyo huu
ndiyo wakati mwafaka wa kumpa lifti kocha Nooij, kwa yule anayeona ana nafasi
ya kuisaidia Stars na kocha huyo basi afanye hivyo ili kampeni hiyo ambayo mara
ya mwisho ilikuwa na mafanikio mwaka 1980, ifanikiwe tena.
Viongozi:
Wapo wengi
wenye nafasi ya kutoa mchango wao, mfano wale wa Yanga, Simba, Azam FC, Mtibwa
Sugar na timu nyingine wanaweza kuwa na mchango wao wa hali na mali na wakaufikisha
TFF.
TFF
wanapaswa kuamini wanaopeleka maoni, hasa viongozi ni wazalendo, hivyo yapokewe
na kusaidia mafanikio ya timu. Mwenye uwezo wa kutoa fedha pia ajitokeze.
Kikubwa,
siasa za soka zikae kando, wasiwepo wapinzani wa Rais wa TFF, Jamal Malinzi wanaoona
timu ikishinda ni mafanikio yake, wakataka kuharibu, hilo lipo!
Wachezaji:
Wachezaji na
memba wengine wa benchi la ufundi wao wana nafasi kubwa zaidi ya kumsaidia
kocha huyo kwa kuyabeba maelekezo yake kwa ufasaha na baada ya hapo wapambane
vilivyo.
Mafanikio
yakipatina, bado sifa itakwenda kwao kutokana na kazi yao nzuri ingawa bado
bosi wao, Nooij atakuwa amefanikiwa pia na itakuwa furaha kwa Watanzania.
Mashabiki:
Utagundua
kila mtu ana nafasi yake ya kuisaidia Stars, naamini hata makala haya
yameisaidia Stars hivyo na mimi nimo!
Kila
Mtanzania ana nafasi hata kama atawakilishwa na wale wanaokwenda mazoezini au
kwenye mechi, bado litakuwa jambo bora.
Sahihi ni
kwenda uwanjani na kuishangilia Stars kwa nguvu, wale ambao wamekuwa wakizomea
wachezaji ni wasaliti. Haitakiwi kuwa hivyo kwa kuwa hakuna mchezaji anayenuia
kukosea.
Ndiyo maana
kuna marekebisho kupitia maelekezo ya mwalimu wakati timu inacheza. Kama kuna
mtu anaizomea timu ya taifa lake ikipambana, basi bora abaki nyumbani na si
kwenda kugeuka kuwa mpinzani mwenye uraia wa Tanzania!
0 COMMENTS:
Post a Comment