June 7, 2014



HARUFU ya mapambano ya Kombe la Dunia 2014 imeanza, kama ni meli inakaribia kutia nanga bandarini na Watanzania na duniani kote wanaisubiri kwa hamu michuano hiyo mikubwa zaidi ya soka itayaofanyika Brazil.
Kati ya vitu ambavyo ni vivutio ni ushindani na ratiba iliyopangwa kutokana na makundi inaonyesha ugumu na kuna mechi kadhaa ndiyo unaweza kuziangalia katika hatua ya kwanza ya makundi, usikose.
Mechi hiyo ni kutokana na historia, ubora wa timu, umahiri wa wachezaji.
Kwa historia, kuna timu zilikutana katika hatua za juu za robo, nusu na fainali lakini safari hii zitakutana kwenye makundi.
Hispania Vs Uholanzi
Jamaa wamekutana kundi B, lakini wao ndiyo walicheza mechi ya mwisho ya Kombe la Dunia mwaka 2010 jijini Johannesburg, Afrika Kusini, Hispania wakashinda 1-0 na kubeba kombe.
Sasa inakuwa ni mechi ya kisasi na itakuwa ni ya ufunguzi kwa kundi hilo kwa kuwa inachezwa Juni 13 ikiwa ni siku moja tu baada ya mechi ya ufunguzi.
Kocha Luis van Gaal ana kazi ya kulipa kisasi na Vicente Del Bosque anataka kuthibitisha Hispania hawakubahatisha na anataka pointi tatu muhimu kusonga mbele.
England Vs Italia
Upinzani wa nguvu ya soka haujaisha kati ya nchi hizi mbili. Mara nyingi zinakutaka kwenye hatua za mtoano lakini sasa ziko Kundi D.
Majina ya wachezaji wanaokutana ndiyo gumzo zaidi, England ina presha ya kusonga mbele lakini Italia wanalijua hilo na siku zote wanataka kuonyesha wao ni bora kuliko England.
Wengi wanaamini Mario Balotelli wa Italia na Wayne Rooney wa England ndiyo watakaotupiwa macho zaidi katika mechi hiyo ya Juni 14.
Ujerumani Vs Ureno
Ngoma itapigwa Juni 16, Kundi G ndilo la ‘kifo’ katika michuano hiyo na ukubwa wa mechi hii ni hadhi kuanzia robo fainali hadi fainali, lakini iko kwenye makundi.
Wajerumani wana kikosi imara na wanataka ubingwa, lakini Cristiano Ronaldo anataka kuweka historia kuingoza Ureno kubeba kombe hilo, angalia namna ngoma itakavyokuwa kali na ya kusisimua.

Marekani Vs Ghana
Katika Kombe la Dunia mwaka 2010 Afrika Kusini, Championi lilishuhudia ‘live’ Ghana ikitinga robo fainali kwa mara ya kwanza baada ya kuifunga Marekani kwa mabao 2-1, muuaji akiwa Asamoah Gyan.
Sasa timu hizo zinakutana Juni 16 kwenye hatua ya makundi, ziko kundi G ambalo limebatizwa jina la ‘kifo’ kutokana na ugumu.
Ugumu wa mechi hii unaipa hadhi ya kuwa zile ambazo zingeweza kuchezwa hatua ya robo au nusu fainali.

Brazil Vs Mexico
Kocha Mkuu wa Brazil, Luiz Felipe Scolari alipoulizwa kama amekuwa akiihofia Mexico katika hatua ya makundi, hakuficha, akafunguka hivi: “Mexico ni timu ngumu na inayotupa wakati mgumu kila tunapokutana nao.”
Kweli Mexico wamekuwa wasumbufu na wababe wa Brazil kila wanapokutana. Katika kipidi karibu karne moja katika timu za Amerika Kusini na hasa katika michuano ya bara hilo, hakuna timu imeshinda mara nyingi dhidi ya Brazil kama Mexico, hivyo hofu lazima ipo mbele ya Wabrazil dhidi ya wagumu hao kutoka Amerika ya kati, mechi itapigwa Juni 17.
Uruguay Vs England
Waingereza wamekuwa wakiendelea kumuombea adui yao njaa, hasa Luis Suarez, wanataka endelee kuwa mgonjwa hadi itakapopita Juni 19 wakati England itakapovaana na wabishi Uruguay.
Wanamjua Suarez ambaye alikuwa mfungaji bora Premieship, alifunga mabao 31. Lakini akikosekana usimsahau Edinson Cavani aliyefunga mabao 25 akiwa na mabingwa wa Ufaransa, PSG.
Marekani Vs Ureno
Upinzani mkubwa wa Marekani na Ureno ambao umepanda kwa asilimia 52 kwa kipindi cha miaka sita tu. Timu hizi ziko kwenye kundi la G ambalo ndilo la ‘kifo’ katika michuano hiyo.
Gumzo hapa, Jurgen Klinsman ataivusha vipi Marekani lakini watu wanataka kuona kazi ya Ronaldo, ngoma hii itapigwa Juni 22.
Uholanzi Vs Chile
Mechi ya Kundi B inaweza isiwe maarufu sana, lakini zitakuwa kati ya zile zenye burudani saafi katika hatua ya makundi.
Chile ni wazima, usiwadharau maana wana wakali kama akina Arturo Vidal na Alexis Sanchez ambao wanalijua vema soka la Ulaya na akina Arjen Robben, Robin van Persie na wenzao kama watazubaa wanaweza kushangazwa na wakali hawa. Isubiriae Juni 23.
 Marekani Vs Ujerumani
Ushindani kati ya Ujerumani na Kocha Klinsiman ambaye ni Mjerumani na aliwahi kuwa kocha na nyota wa timu hiyo.
Aliiongoza Ujerumani kushika nafasi ya tatu kwenye Kombe la Dunia mwaka 2006 kwenye udongo wa nyumbani, sasa anapambana nayo akihakikisha anataka kuwashinda akina Thomas Muller, Bastian Schweinsteiger, Mesut Ozil na wengine lakini Marekani pia ina akina Omar Gonzalez, Matt Besler na wengine kibao. Si kitu kidogo.
Fin.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic