Kocha Mkuu wa Yanga, Mbrazili, Marcio
Maximo, amekabidhi mapendekezo ya usajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu
Bara huku akitaka wachezaji wenye uwezo wa kimataifa.
Maximo alitua juzi Alhamisi
jijini akiwa ameongozana na msaidizi wake, Leornado Leiva kwa ajili ya kukinoa
kikosi hicho kinachojiandaa na Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
Amesema usajili wa wachezaji wake lazima uwepo mchanganyiko
wa mataifa mbalimbali, ikiwemo Ulaya.
Maximo alisema, lengo la usajili huo
ni kutengeneza kikosi imara na chenye uwezo wa kucheza mashindano ya kimataifa
ili wafanye vizuri.
Katika kukiimarisha
kikosi amepanga kutengeneza msingi mzuri wa kuwandaa wachezaji kwa kuunda
kikosi imara cha U20 kitakachokuwa chini ya msaidizi wake, Leiva.
Pia amepanga kuanza kukinoa kikosi
hicho keshokutwa Jumatatu kwa kuanza na programu ya mazoezi ya nguvu.
“Tayari nimekabidhi mapendekezo ya usajili
wangu kwa Kamati ya Utendaji ya Yanga, kikubwa ninataka wachezaji wenye uwezo
wa kucheza mashindano ya kimataifa.
“Katika usajili wangu lazima uwepo na
mchanganyiko wa wachezaji kutoka mataifa mbalimbali kwa kuanzia Afrika na
Ulaya.
“Lengo ni kuleta mchanganyiko wa aina
ya soka kutoka mataifa mbalimbali, haiwezekani timu iundwe na wachezaji
Watanzania pekee, alisema Maximo na kuongeza:
“Kwa nini TP Mazembe yenyewe iwe
inajulikana kimataifa? Haiwezekani, hivyo lazima na sisi tufikie historia nzuri
kama waliyokuwa nayo hao kwa kuchukua makombe mbalimbali Afrika.”
Aidha, aliongeza kuwa, anaufahamu vizuri
ushindani wa ligi uliopo ambapo hivi sasa umeongezeka, hasa kutoka kwa timu za Azam
FC, Mbeya City, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar.
Alipoulizwa Katibu Mkuu wa Yanga, Beno
Njovu kuhusiana na mapendekezo hayo, alisema: “Ni kweli tumepokea mapendekezo
ya usajili wa wachezaji anaowataka Maximo, tayari yamefika kwa uongozi
mapendekezo yake hayo.
“Ripoti hiyo
tumeipitia, lakini tutaangalia kama mapendekezo hayo yataambatana na kanuni za
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).”
0 COMMENTS:
Post a Comment