Winga mkongwe wa Ashanti United, Said
Maulid ‘SMG’, amesema atajisikia faraja na furaha tele iwapo atamaliza soka
lake akiwa anaitumikia Yanga.
SMG amesema kuwa
anaiheshimu Yanga kama klabu iliyomtambulisha zaidi kwenye ulimwengu wa soka,
hivyo anaamini akirudi na kustaafu hapo itakuwa ni heshima kubwa kwa upande
wake.
Hata hivyo, mchezaji huyo ambaye
amemaliza mkataba wake wa kuitumikia Ashanti msimu uliopita, amesema bado ana
uwezo mzuri wa kucheza hata kwa miaka minne zaidi lakini anaweza akastaafu soka
hata baada ya mwaka mmoja kama azma yake hiyo itatimia.
“Sijajua bado msimu ujao nitachezea
timu gani lakini nakwambia ukweli kwamba natamani sana nistaafu soka langu nikiwa
naichezea Yanga, hili linatoka moyoni.
“Yanga ni timu ninayoiheshimu sana kwa
sababu ndiyo imenitambulisha zaidi kisoka hapa Afrika, itakuwa ni heshima na
faraja kubwa kwangu mimi binafsi kama nikistaafu nikiwa na jezi ya klabu
ninayoiheshimu zaidi.
“Bado nina nguvu ya kucheza soka hata
kwa miaka minne ijayo lakini kama itatokea Yanga itanisajili hata kwa mwaka
mmoja, basi mwaka huohuo na mimi ndiyo nitastaafu kuonyesha jinsi gani nataka
kutimiza dhamira yangu,” alisema SMG anayesifika kwa kuwa na kasi kubwa
uwanjani.
SMG alitua Yanga kwa mara ya kwanza
akitokea Simba mwaka 2002 na kuitumikia mpaka mwaka 2008 alipokwenda kukipiga
kwenye Klabu ya Onze Bravos Dos Maquis ya Angola kabla ya kurejea kujiunga na
Ashanti mwaka jana.
0 COMMENTS:
Post a Comment