July 2, 2014



Na Saleh Ally
NILIKUWA nimebeba kamera yangu nyuma ya lango la Uruguay, ilikuwa ni mechi yangu ya nne kupiga picha kwenye michuano mikubwa kabisa ya Kombe la Dunia.


Hiyo ilikuwa mwaka 2010 wakati Ghana ilipokuwa ikipambana na Uruguay katika mechi ya robo fainali kuwania kuwa timu ya kwanza Afrika kucheza nusu fainali ya Kombe la Dunia. Lakini mpira wa kichwa uliokuwa unakwenda kuvuka mstari wa lango la Uruguay, ulidakwa na mshambuliaji Luis Suarez.

Akalambwa kadi nyekundu, akatoka. Lakini bahati mbaya hata mshambuliaji wa Ghana, Gyan Asamoah, aliyepewa nafasi ya kupiga mkwaju ule, takribani mita 30 kutoka nilipokuwa, naye akapaisha mpira ule, yote nikamuachia Mungu.

Lakini nikiwa njiani kurejea katika Jiji la Johannesburg, nilipoishi kwa mwezi mzima nikiripoti michuano hiyo, nilikuwa na maswali mengi sana. Nilipata nafasi ya kutafakari kwa muda mwingi kwa kuwa kazi ya kuendesha gari kwa safari ya kurejea nilipokuwa ninaishi ilikuwa ni ya rafiki yangu, nikapitiwa usingizi.

Niliposhtuka, ndiyo rafiki yangu alikuwa akiegesha gari kwenye mgahawa wa KFC ili tupate nafasi ya kula. Bado niliendelea kuwaza kuhusiana na Suarez, kwamba kweli ni shujaa kwa nchi yake, lakini aliwavuruga Ghana na Afrika.

Tafakari yangu kuhusiana na mtu huyo haikuwa na kipimo cha kutosha, niliendelea kuamini hakuwa mtu mzuri, mbinafsi, anayetaka chake bila kujali cha wengine. Mwisho nikasema wanadamu kukosea ni kawaida.

Kabla ya hapo, tayari alikuwa ‘anashikilia’ tukio moja la kumng’ata mchezaji, Ottman Bakkal wa PSV Eindhoven wakati akiichezea Ajax, hiyo ilikuwa katika Ligi Kuu ya Uholanzi. Naye binadamu, nafsi yangu ikanifanya niamini bado ni makosa ya kibinadamu.

Lakini baada ya hapo Suarez akiwa na kikosi chake cha Liverpool akaingia kwenye kashfa nyingine baada ya kumbagua beki wa Manchester United, Patrice Evra kwa kuwa ni mweusi, nikaendelea kuwa na maswali.

Wakati hilo linapoa na watu wanajaribu kusahau kama ilivyo ada ya binadamu, Suarez akaingia kwenye kashfa nyingine ya kumuuma beki wa Chelsea, Blanislav Ivanovic wakati akiwa hana hata mpira.

Hili lilikuwa ni jambo la kushangaza ingawa hakuwa amefanya kwa mara ya kwanza. Wakati hilo ndiyo limepoa na Suarez amemaliza msimu wa 2013-14 kwa kishindo, pia kuanza Kombe la Dunia, sawa kwa kuimaliza England na kuing’oa kwenye michuano hiyo, kafanya upuuzi mwingine tena.

Safari hii akamuuma beki Giorgio Chiellini wa Italia, hawakuwa wanagombea mpira, kila mtu alikuwa amesimama sehemu yake. Bila ya huruma akapitisha meno yake ‘njino’ kwenye bega la beki huyo.

Sitaki kuendelea kushangazwa ingawa nimegundua hata wapuuzi wana watu wao wa kuwaunga mkono kama ambavyo ilitokea kwa Waruguay hadi mkuu wa nchi yao kuonyesha si wale wanaoamini ‘Fair Play’ kutokana na kulalama eti Suarez anaonewa.

Akapokewa kama shujaa aliporejea Montevideo, mashabiki wakajaa kwenye nyumba yake kumuunga mkono na hata uongozi wa kikosi cha Uruguay ukapinga Fifa kumuondoa kwa kuweka jezi yake kwenye chumba cha kubadilishia nguo katika mechi yao dhidi ya Colombia ambayo walikiona cha moto.

Kocha wake, Oscar Tabarez, akajitoa kwenye kamati ya ufundi ya Fifa, eti anapinga kuonewa kwa mchezaji wake. Lakini wote wameonekana ni wapuuzi baada ya Suarez kuomba radhi.

Kupitia Mtandao wa Kijamii wa Twitter, Suarez ameomba radhi, amekubali alichokifanya ni upuuzi, amemuomba radhi Chiellini na wapenda soka wengine. Ameahidi hatarudia upuuzi alioufanya.

Baada ya msamaha huo wa Suarez, kwangu nimejifunza zaidi ya kile cha kwanza kwamba hata wapuuzi huwa wana watu wa kuwaunga mkono. Ndiyo maana wapo waliomshangilia Suarez, wengine ni raia wa Tanzania, ni kutokana na ushabiki wao tu, hawakujali kiasi gani mtu huyo anauvuruga mchezo wa soka.

Kwa miaka mitatu, Suarez ndiye amekuwa binadamu anayeongoza kupingana na ‘Fair Play ‘kuliko binadamu mwingine yeyote tangu mchezo wa soka uanze kutumia sheria zinazoelekeza uchezwe vipi, kiungwana.

Soka si vita, haulengi kuumizana, sasa vipi mchezaji wa kiwango cha juu kama Suarez afanye mambo ambayo hata kwenye mechi za mchangani hapa Tanzania hauwezi kuyaona, halafu wapo wanaomuunga mkono? Eti utaifa!

Ukiangalia wakati anakwenda kumuuma Chiellini, utagundua Suarez alipania, maana amekimbia zaidi ya hatua nne kabla ya kumfikia na kumuuma begani wakati akiwa hana mpira wala hagombei chochote dhidi yake. Huyu ni wa namna gani?

Lakini sasa anaomba radhi kwa kuwa tu anataka kujisafisha kwa maslahi yake, maana ameambiwa Barcelona inamhitaji kwa kitita cha pauni milioni 80 (zaidi ya Sh bilioni 227) baada ya Liverpool kuonyesha iko tayari kusahau ubora wake na kumuachia kwa kuwa inahofia tabia zake hizo!

Suarez ndiye mwanasoka mbinafsi, mbaguzi, mwenye roho mbaya kuliko wengine wote waliowahi kutokea duniani katika kipindi cha muongo mmoja. Anajali maslahi yake, hajali utu hata kidogo.

Ingekuwa ni filamu, kila mara angeigiza kama kubwa la majambazi. Lakini utaona kiasi gani anavyotoa somo kwa vijana ambao leo wataamini unaweza kuwa mtovu wa nidhamu lakini ukavutia klabu kibao kutokana na kipaji chako.

Angalia alivyo kigeugeu, alifika Montevideo kama shujaa kwa kumuuma mwenzake, hakusema lolote, watu wakamsapoti hadi kocha wake. Leo, amewageuka hata wao, kuomba radhi maana yake wote walifanya upuuzi kusapoti ujinga wake. Hajali hilo kwa kuwa sasa yupo kimaslahi!

Sina swali tena kutokana na nilichokuwa nakifikiria miaka minne iliyopita nchini Afrika Kusini. Nakuwa mmoja wa watu niliowahi kushuhudia ubinafsi wa Suarez 'live', lakini sitajiuliza tena kuhusu yeye.

Tumekuwa tukilia na tabia hasi za wachezaji wa Kitanzania na Afrika, lakini mfalme wao ni Suarez ambaye ni mtu hatari kwa afya ya mchezo wa soka duniani. Bahati yake siwezi kuandika kwa lugha yao!

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic