Na Saleh
Ally
TANZANIA
ndiyo tumekwama Kombe la Dunia, huenda mimi na wewe ambao tuna kati ya miaka 25
hadi 35, tutaendelea kulishangilia kwa kujichagulia nchi za wenzetu hadi hata
kama Mwenyezi Mungu atatujaalia kufikisha miaka 80.
Usiseme
natanguliza uchuro, lakini jiulize mipango iko wapi ambayo unaweza kuiita
madhubuti kwamba itafikia siku na sisi tutakwenda kucheza michuano hiyo mikubwa
ya soka duniani.
Kila baada
ya miaka minne, Kombe la Dunia linafanyika, sisi ‘ayaaa’, ilibaki kidogo
tuende, halafu miaka mingine minne, tunarudia hayohayo bila ya kuona haya hata
chembe.
Kila
kiongozi anayeingia anakuwa na mipango yake, haiendani na yule aliyemaliza muda
wake, maana yake kila baada ya muda tunakuwa na mipango mipya, si endelevu.
Maana yake tutasubiri bila kupata na watu wanaona poa tu!
Sikioni
anachokifanya Jamal Malinzi wa TFF, unaweza kusema tutakuwa na uhakika wa
kushiriki Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi. Mwisho tutajisikia, aah ilibaki
kidogo tu au kisingizio tunaonewa.
Lakini
hatuna tofauti na wale ambao wanafuzu kwenda kwenye michuano hiyo, wanaonyesha
ndani ya Afrika kuna matatizo makubwa na hata kama tutapata nafasi ya kushiriki
kwa timu zetu tano, tutaendelea kufeli.
Afrika ina
nafasi tano, usisahau Tanzania haijawahi kupata, lakini wanaopata nafasi hizo,
wengi wanaonyesha bara hili lina uwezo mkubwa wa vipaji vya soka, lakini
matatizo ni mawili, fedha na nidhamu.
Fedha kwa
maana ya kupata kila kinachotakiwa ndiyo maana wanaofanya vizuri wakiwa na timu
zao kwenye Kombe la Dunia, wanatokea barani Ulaya au kwingineko. Unaweza
kujiuliza hivi, vipi Asia wenye timu nne nao walifeli kupitisha hata timu moja
kwenda 16 bora?
Afrika
ilipitisha mbili, Algeria na Nigeria na zote zimeng’olewa? Jibu hapa kuna mambo
mawili pia, kuzidiwa uwezo kutokana na ubora wa wenzetu. Ila Nidhamu ndiyo
limekuwa tatizo kubwa sana, nitaeleza.
Cameroon,
waligombea posho, wakagombana kambini, mmoja wa wachezaji wao Alex Song,
akamtwanga mtu ‘kipepsi’ hata hana mpira!
Ivory
Coast, kumekuwa na mgogoro wa chinichini, inaonekana tayari kuna makundi kati
ya wakongwe na wale chipukizi ambao alikuwa anawaamini zaidi kocha Sabri
Lamouch. Mwisho wametolewa kama wengine.
Ghana,
hakuna anayeweza kukataa kwamba walikuwa na kikosi bora kabisa, bahati mbaya
wakaangukia katika kundi gumu dhidi ya Ujerumani, Ghana na Marekani lakini bado
walionyesha kiwango.
Katikati ya
mapambano, Sulley Muntari akamtwanga kiongozi, Prince Boateng akaanzisha
tafrani, wote wakatimuliwa. Kikosi kizuri lakini nidhamu mbovu na hakuna
tofauti na wengine.
Angalia Nigeria
na Algeria, wameonyesha mfano, ndiyo maana walifanikiwa kufika hata 16 bora.
Nidhamu imewavusha kwa kuwa ukisema timu bora, zile tatu zilizotoka mapema
ndiyo zilipewa nafasi ya juu zaidi kuifikisha mbali Afrika.
Nigeria na
Algeria ndiyo walionekana hawana nafasi kwa maana ya uwezo wa vikosi vyao,
ukiangalia majina au wale wachezaji wakubwa.
Lakini
wamekwenda mbali zaidi kuliko waliopewa nafasi kutokana na kuwa na uwezo na
wenye majina makubwa. Hii ndiyo maana sahihi ya nguvu ya nidhamu katika mchezo
wa soka.
Watanzania
tunalilia kwenda Kombe la Dunia, lakini tuamini inawezekana nidhamu ya chini ya
viongozi wa shirikisho, klabu zetu na wachezaji wenyewe pia inaweza ikawa
inatuangusha.
Nidhamu ni
udhaifu mkubwa katika mambo mengi barani Afrika, hakuna ubishi hata nyumbani
Tanzania huo ndiyo udhaifu wa wengi, taasisi nyingi na mwisho tunajikamua
kutupia watu lawama bila ya kujikagua.
Tusiache
mifano hii ikapita tu, tujifunze kuwa inawezekana kabisa kufanikiwa kwa uwezo
wa fedha na kipaji. Lakini nidhamu inaweza ikawa ni nguzo ya kubadilisha mambo
na mwisho ikawezekana tukacheza Kombe la Mataifa Afrika na baadaye Kombe la
Dunia.
0 COMMENTS:
Post a Comment