Na Saleh
Ally
WATANZANIA
wanaweza kuwa mashuhuda si kwa kuangalia kwenye ‘kideo’ badala yake wataeleza
umahiri alionao mshambuliaji, Didier Drogba kwa kuwa amewahi kuzitikisa nyavu
za Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Drogba
alifunga bao pekee wakati Taifa Stars ilipolala kwa bao 1-0 katika mechi ya
kirafiki iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Ufundi wa
bao lile, aliwahi kuhadithia beki kisiki nchini, Nadir Haroub ‘Cannavaro’
aliyeeleza wepesi wa Drogba na akili ya haraka linapofikia suala la kufunga.
Drogba sasa
ana umri wa miaka 36, lakini kocha Jose Mourinho wa Chelsea, ameshindwa kuficha
anachokiamini ndani ya moyo wake, ameamua kumrudisha mkali huyo kundini.
Drogba
amesaini kuichezea Chelsea kwa mwaka mmoja akitokea Galatasaray ya Uturuki,
hali ambayo imewafanya wengi wajiulize maswali, kila mmoja akiwa na upande
wake.
Wapo wanaohoji
kama kweli Drogba atakuwa na makali kama yale alipoichezea Chelsea kuanzia
mwaka 2004 hadi 2012 alipoamua kuondoka. Wengine wanahoji kuhusu Mourinho
kuamua kujaribu patapotea hiyo na kama itakuwa na msaada kwake.
Kuna mambo
mengi aliyonayo Drogba ambayo yangeweza kumshawishi kocha yeyote makini na
kuamini kweli atafanya vizuri na kufanikiwa akiwa na Drogba.
Mourinho si
mgeni kwa Drogba na hakuna shaka anajua anachokitaka na ‘Tembo’ huyo anaijua
kazi yake kwa kuwa kuanzia akiwa na umri mdogo hadi ‘uzeeni’ bado ameendelea
kuthibitisha kuwa ni kiwembe.
Ukiwembe wa
Drogba si wa maneno, unadhihirishwa na takwimu ya timu zote alizopita na ligi
alizozichezea kwamba si mtu wa kuchezea, silaha yake kubwa ni kazi ya ukweli.
Kwa msimu
mmoja akiwa na Chelsea, bado ana nafasi ya kutoa msaada na vizuri atakuwa na
‘ticha’ anayejua afanye nini akiwa naye. Yaliyomvuta Mourinho ni mengi na inawezekana
asifanye vizuri lakini kufanya vizuri zaidi ni asilimia nyingi. Angalia baadhi
ya haya.
Mabao 100:
Hadi
anaondoka Chelsea, Drogba aliweka rekodi ya kuwa Mwafrika wa kwanza kufunga
mabao 100 katika Ligi Kuu England, maarufu kama Premiership.
Drogba aliondoka
na mabao 100 kamili baada ya kuichezea Chelsea mechi 226. Amekuwa mchezaji wa
22 kufunga mabao 100 katika ligi hiyo. Kocha yeyote angeweza kuvutiwa naye.
Kila timu:
Wastani wa
mabao aliyofunga kwa kila timu aliyoichezea kuanzia mwaka 1998, inaonyesha ni
mshambuliaji mwenye uwezo wa juu sana. Angalia jedwali.
MWAKA
TIMU MECHI/MABAO
1998–2002
Le Mans 64(12)
2002–2003
Guingamp 45(20)
2003–2004
Marseille 35(19)
2004–2012
Chelsea
226(100)
2012–2013
Shanghai 11(8)
2013–2014
Galatasaray 37(15)
2014–
Chelsea ?(?)
Eto’o:
Ilionekana
Samuel Eto’o ndiye angeziba pengo na kuwasahaulisha Chelsea kuhusiana na
Drogba. Lakini inaonekana imeshindikana na sasa amerejea.
Bado atakuwa
na mtihani mkubwa wa kuonyesha Mourinho hakukosea, lakini pia kufanya kazi
nzuri zaidi ya ile iliyofanywa na ‘shemeji’ yake Eto’o akiwa na Chelsea kwa
msimu mmoja. (Mke wa Eto’o ni raia wa Ivory Coast).
Makombe:
Kwa misimu
miwili aliyocheza Uturuki akiwa Galatasaray, Drogba amefanikiwa kutwaa makombe
matatu ya ligi kuu (2012–13), Super Cup (2013) na Kombe la Uturuki (2014).
Sasa
kumbuka kipindi cha Chelsea wakati akiwa na Mourinho na hata baada ya hapo,
Drogba amekuwa akibeba tu makombe.
Hadi
anaondoka Chelsea, amefanikiwa kubeba jumla ya makombe 10 ya Ligi Kuu England,
Kombe la FA na Kombe la Ligi. Pia amebeba ngao mbili za jamii.
Maana yake
anaporudi leo Chelsea, inaonekana Mourinho ana haki ya kujaribu tena kama
almasi aliyojipamba nayo miaka kadhaa iliyopita, kweli bado inaweza kung’ara?
Ikishindikana,
basi hakuna anayeweza kumcheka kwa kuwa hata kama kweli ni masharti na vigezo,
amezingatia na kazi ya Drogba ndiyo iliyomtia wazimu. Kikubwa sasa ni kusubiri,
Drogba ataweza? Kwa kuwa mpira unachezwa hadharani, acha Premier League ianze.
0 COMMENTS:
Post a Comment