Kocha mkuu
wa timu ya Yanga Mbrazili, Marcio Maximo ni kama vile sasa ameamua kuwatolea
uvivu wachezaji wake wa kimataifa wa Uganda Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza
kutokana na kile alichosema juu ya aina ya wachezaji anaowahitaji katika kikosi
chake na yupo tayari kuwatema.
Kwa sasa ndani ya klabu ya Yanga kuna mchako wa kupunguza mchezaji mmoja
wa kimataifa ili kupata nafasi ya kumuongeza katika usajili wao Mbrazil
Genilison Santos ‘Jaja’ aliyeingia mkataba wa miaka miwili.
Sheria ya soka la Tanzania inaitaka kila klabu inayoshiriki Ligi Kuu
Bara kuwa na wachezaji watano wa kimataifa, lakini Yanga mpaka sasa ina
wachezaji sita, Kiiza, Okwi, Jaja, Andrey Coutinho, Mbuyu Twite, Haruna
Niyonzima.
Maximo amefunguka kuwa kamwe hatakubali kufanyakazi na mchezaji mbinafsi
na mwenye chuki kwenye kikosi chake na yupo tayari kumtema hata kama atakuwa na
kiwango gani.
Kauli hiyo, ni kama inawagusa viungo Okwi na Kiiza ambao wenyewe kila
mara wamekuwa wakilalamikiwa na vitendo hivyo na viongozi wa juu wa timu hiyo.
Katika msimu uliopita wa ligi kuu, Okwi alidaiwa kugomea kucheza mechi
sita mfululizo ambazo zote zilikuwa muhimu ikiwemo dhidi ya Simba na Azam FC.
Wakati Okwi akifanya tukio hilo, Kiiza mwenyewe alionyesha utovu wa
nidhamu kwa kuondoka kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na kwenda kukaa
jukwaani mara baada ya kutolewa nje na aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hans
Pluijm timu hiyo ilikuwa ikivaana na Ruvu Shooting.
Mbali na hayo Kiiza kuna kipindi aligoma kucheza Yanga, kutokana na
madai kuwa amepata timu na Yanga wanambania kwenda huku akishutumiwa kwa
ujeuri, huku Okwi usumbufu wake ulianzia alipokuwa katika timu ya Simba ambapo
mara kwa mara alikuwa akikorofishana na viongozi wake.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Maximo alisema kuwa kila mchezaji
kwake ni sehemu ya ushindi, hivyo hatakubali kuona makundi yakitengenezwa
kwenye kikosi chake ambayo yatasababisha mgawanyiko.
Maximo alisema, amekubali kuifundisha Yanga kwa ajili ya kuibadilisha na
kuipa mafanikio makubwa ikiwemo timu kushinda na kuchukua mataji ya ubingwa
mbalimbali.
Aliongeza kuwa, pia katika kikosi chake hatampanga mchezaji kutokana na
ukubwa wa jina, atampa mchezaji nafasi ya kucheza yule anayejituma na
anayetambua majukumu yake ndani ya uwanja katika kupata ushindi.
“Mchezaji mbinafsi na mwenye chuki, kamwe sitampa nafasi ya kucheza
kwenye kikosi changu, kikubwa ninachoangalia ni uwajibajika wa mchezaji ndani
ya uwanja, lakini wale wenye utovu wa nidhamu nitaachana nao.
“Silaha kubwa ya ushindi katika timu ni amani na upendo, hivyo ili timu
ipate ushindi na ichukue makombe basi umoja lazima uwepo na siyo kuwepo na
ubinafs na chuki huku wengine wakijiona wao ndio kila kitu.
“Hivyo kama nikimgundua au nikiwagundua wachezaji wenye tabia hizo, basi
nitaondoa kwenye kikosi change haraka sana, bado nawafatilia wote na nasubili
hao wengine waje ndiyo nitatoa msimamo wangu wa mwisho, ni vyema wachezaji
wangu wote wakalifahamu hilo,”alisema Maximo.
Maximo ni kati ya kocha anayetambulika kusimamia nidhamu ya hali ya juu
katika kila timu anayofundisha, anakumbukwa kwa jinsi alivyowatema mastaa kama
Juma Kaseja, Athuman Iddy ‘Chuji’ na Haruna Moshi ‘Boban’ alipokuwa kocha wa
Taifa Stars miaka sita iliyopita.
Wakati huohuo uongozi wa Yanga umeamua kukaa kando kuhusu kupunguzwa kwa
mchezaji mmoja wa kimataifa klabuni hapo na sasa umemakabidhi rasmi suala hilo
Maximo aamue moja kati ya Okwi na Kiiza.
Kutokana na kauliza Maximo, Championi Jumamosi lilizungumza na Katibu
Mkuu wa Yanga, Beno Njovu na kufafanua kuwa hiyo ishu ya kiufundi zaidi na
kwamba wao kama uongozi hauwezi kuiingilia badala yake wamemwachia Maximo ndiyo
atakayekuwa na maamuzi ya mwisho kuhusiana na hilo.
“Unajua haya ni mambo ya kiufundi zaidi kuhusu kuchagua ni wachezaji
gani wabaki na nani aondoke kwa ajili ya msimu ujao, kocha mwenyewe ndiyo
ataangalia wakina nani watamfaa na nani hamfai kisha yeye atatoa maagizo
kulingana na tathimini yake.
“Yeye anatambua kuhusu usajili wa wageni na ndiyo aliyetoa pendekezo la
usajili wa Jaja na Coutinho kwa hiyo tayari ana ‘target’ zake, tumwache aamue
yeye anaotaka wawepo kwenye mpango wake kisha sisi tutatekeleza, hatuwezi
kumpangia,” alisema Njovu.
Tangu Maximo aanze kuinoa Yanga takriban wiki nne
zilizopita mpaka sasa Kiiza, Okwi na Niyonzima bado hawajajumuika kwenye mazoezi
ya timu hiyo kutokana na majukumu ya timu zao za taifa waliyokuwa nayo lakini taarifa zinaeleza kuwa tayari
Maximo ameshaangalia CD za wachezaji hao kwa ajili ya kuufahamu uwezo wao.
0 COMMENTS:
Post a Comment