August 27, 2014





Na Saleh Ally
BAADA ya Mario Balotelli kutua Liverpool, moja kwa moja  akaomba apewe jezi namba 45, ambayo amekuwa akiitumia kuanzia akiwa kinda pale Inter Milan ya Italia.


Kawaida, Inter Milan, inatoa nafasi kwa wachezaji makinda kuchukua namba 36 hadi 45 hasa kwa wale waliopandishwa kwenye kikosi cha kwanza.

Baloteli alichukua 45, lakini amekataa kuibadili kila anapokwenda, kwani hata akiwa Manchester City alikuwa akiitumia.

Mwenyewe anasisitiza kwamba ingawa 4 ikiwekwa na 5 inaonekana ni 45, huo ni muonekano wa macho yaw engine. Yeye anaitazama hivi 4 ikijumlishwa na 5, pale mgongoni mwake kunakuwa na namba 9 ambayo ndiyo anayoipenda. Balotelli haishi vituko.

Kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Manchester City, ambacho walikipata Liverpool usiku wa kuamkia jana kinathihirisha kwamba kweli Kocha Brendan Rodgers, alikuwa anahitaji mshambuliaji wa kati msumbufu.


Liverpool ilionekana haikuwa na madhara makubwa sana mbele ya mabeki wakubwa na wababe wa Manchester City ambao hawakuwa na kazi kubwa huku Daniel Sturridge na Raheem Sterling wakionekana wakiwa wamezidiwa mzigo.

Kiungo wake Mbrazil, Coutinho pia alionekana kushindwa kufiti katikati huku akipoteza pasi nyingi mfululizo, hivyo  kutoa nafasi ya Yaya Toure kuiadhibu Liverpool alivyokuwa akitaka yeye kufanya.

Kusema Liverpool haina kikosi kizuri kwa kuwa imeondokewa na Luis Suarez aliyejiunga na Barcelona ya Hispania haitakuwa sahihi lakini kwamba inahitaji huduma ya Balotelli, hilo halina ubishi.

Wachambuzi wengi wa England wameshangazwa na uamuzi wa kumrudisha Balotelli tena nchini humo baada ya kuwa ameondoka Manchester City na kujiunga na AC Milan ya kwao Italia.

Kawaida Waingereza ni watu wanaopenda kujivunia vya kwao na kuponda vya wenzao, hivyo wangefurahi kuona Liverpool inamsajili mshambuliaji nyota mwenye asili ya England na huenda Wayne Rooney angekuwa sahihi lakini Manchester United isingekubali.

Maana yake, Liverpool walikuwa lazima wafunguke kwingine zaidi na ndiyo Rodgers akaamini Balotelli ni sahihi si kwa kuangalia vituko vyake nje ya uwanja, badala yake ndani ya uwanja kwa maana ya uwezo.

Italia:

Hakuna anayeweza kusema kuwa Liverpool wamekurupuka na kuchukua mtu asiyekuwa na uwezo sahihi wa kukiongoza kikosi chao kwa kuwa Balotelli ndiye mshambuliaji namba moja wa kikosi cha timu ya taifa ya Italia ‘Azzuri’.

Kutegemewa na Italia iliyojaza rundo la vipaji vya soka, maana yake ana ubora wa hali ya juu na anapaswa kutegemewa na timu yoyote katika ligi yoyote ya Ulaya au kwingineko duniani.

England:
Katika msimu wa 2012-13, ambao ulikuwa wa mwisho kwake kuichezea Manchester City na pia AC Milan, Balotelli alicheza jumla ya mechi 39 katika mashindano yote, hicho ni kiwango cha juu cha mchezaji anayeaminiwa na kocha.

Katika mechi hizo 39, alifanikiwa kufunga mabao 20 ambayo yanakwenda kwenye wastani wa juu kwa kuwa imevuka asilimia 50, hivyo hakuwezi kuwa na hofu ya suala la uwezo wake.

Katika mechi hizo, 30 aliichezea Manchester City na tisa akakipiga akiwa na AC Milan, maana yake hapa unapiga hesabu za ligi mbili na kila timu imempa nafasi kutokana na kiwango chake kuwa cha juu.

Nidhamu:

Ndiyo imekuwa hofu kuu ya karibu kila mmoja, ingawa Liverpool wametambua zaidi uwezo au kipaji chake. Hivyo walichokifanya ni kuangalia nini cha kufanya mapema, wakaongeza kipengele cha msisitizo wa suala la nidhamu, jambo zuri zaidi.

Uwanjani bado Balotelli ana matatizo, huenda hili lisiwe kwenye mkataba lakini atalazimika kujichunga. Kwani akiwa na Manchester City, pamoja na kufanya vema lakini rekodi zilimbana kama mchezaji mtukutu kwa kuwa katika mechi 39 alizocheza aliibuka na jumla ya kadi 13. Kati ya hizo 12 zilikuwa  za njano na moja nyekundu.

 Kwa kikosi cha Liverpool kilivyo, kama Balotelli ataamua kubadilika na kucheza soka, hakuna ubishi ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi na kuwa msaada sahihi katika kikosi hicho. Mengi ya nini kitatokea, yanamtegemea yeye zaidi.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic