Unaweza kusema kumekucha
baada ya Yanga kufikia uamuzi wa kumfungulia mashitaka mshambuliaji wake
Emmanuel Arnold Okwi afungiwe kucheza soka.
Yanga imefikia uamuzi huo
baada ya kuonekana kutoridhishwa na mwenendo wa Okwi raia wa Uganda ambaye hata
hivyo ameishatua nchini akisubiri kujiunga na kikosi cha Yanga ambacho kipo
kambini mjini Zanzibar.
Barua ya Yanga ya Agosti 25
iliyosainiwa na Katibu Mkuu, Beno Njovu, imetua kwenye Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) ikifafanua mambo mengi ikiwa ni pamoja na Okwi kukiuka mkataba
na Yanga kwa kufanya mazungumzo na klabu ya WadiGalde FC ya Misri.
Barua hiyo inaeleza Okwi
amekiuka vipengele vya Fifa, Caf na TFF kwa kufanya mazungumzo na timu hiyo ya
Misri ambayo tayari imeiandikia Yanga barua ikitaka kumnunua kwa dola 60,000
(zaidi ya Sh milioni 95).
“Okwi aliwasiliana na mmoja
wa viongozi na kumuambia amefanya mazungumzo na timu ya Misri inamtaka,
kiongozi akamuambia aandike barua, kweli akafanya hivyo kupitia mwanasheria
wake.
“Siku chache baada ya Yanga
kupokea barua, WadiGalde FC nayo ikaiandikia Yanga barua kuwa inamtaka kwa
kitita cha dola 60,000 ambazo zinalingana na zile zilizoandikwa kwenye barua ya
mwanasheria wake. Kulingana kwa kiwango cha fedha kunaonyesha walikuwa na
mawasiliano.
“Hili ni kosa kisheria kwa
kuwa Okwi bado ana mkataba na Yanga, angalau ingekuwa imebaki miezi sita
angeweza kufanya hivyo. Mwanasheria wake (Edgar Agaba) pia ameshiriki na tunaomba
TFF kuwafungia wote kujishughulisha na soka nchini,” ilieleza sehemu ya barua
hiyo.
“Pamoja na kuwafungia, Okwi
anatakiwa kutulipa fidia ya dola 200,000 kwa kuchangia kutukosesha ubingwa
pamoja na kurudisha fedha zote alizolipwa za usajili ambazo ni dola 60,000 pia
fedha zote za mshahara,” ilifafanya zaidi sehemu ya barua hiyo.
Yanga imemtuhumu Okwi kwa
kukosa mechi saba kati ya 13 za mzunguko wa pili kitu kinachoonekana ni kama
kuchukuliwa fedha zake bure kwa kuwa Okwi hakuitumikia ipasavyo.
Msisitizo umewekwa kuwa
Okwi alitoroka kambini hali ambayo ilionyesha utovu wa nidhamu na baadaye
akajiondoa kabisa katika kikosi kwa madai hakupewa nyumba na hakuwa amelipwa
sehemu ya fedha zake zilizobaki.
Hakuna kiongozi wa Yanga au
TFF aliyetaka kulizungumzia suala hilo, lakini Salehjembe ikaamua
kulipaisha kwa kuwa ina uhakika wa asilimia 100 kutokana na kunasa kopi ya
barua hiyo, mara tu baada ya kutua TFF.
Katika barua hiyo ambayo
imetaja vifungu kadhaa vya Fifa ambavyo Okwi amekiuka, maana yake ni
utuhibitisho tosha kwamba sasa haimtaki tena Okwi.
Ile nafasi moja waliyokuwa
wakigombea na Hamis Kiiza, maana inakwenda kwa Mganda mwenzake na yeye anaanza ‘mgogoro’
huo na Yanga ambayo imeamua kuwa ngangari.
Okwi aliyesajiliwa Yanga kwa
dau la dola 100,000 (zaidi ya Sh milioni 165), aliamua kususa kuichezea Yanga
akidai kucheleweshewa fedha na alikosa mechi nne za mwisho za mzunguko wa pili,
zikiwemo mbili dhidi ya Yanga na Azam FC ambao waliibuka kuwa mabingwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment