Suala la Emmanuel Okwi kutangaza kuwa Yanga
imevunja mkataba wake na sasa ataitumikia Simba, limezua sekeseke na sasa ni
mtafutano kila kona, kama ni vita sasa hii ndiyo inaanza kukolea.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, amefunguka
kuwa wametoa siku saba kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa majibu
sahihi juu ya Simba kumtangaza Okwi kuwa mchezaji wao wakati bado kuna kesi
inayoendelea baina ya Yanga na Okwi.
Kuonyesha kuwa wapo ‘serious’ na hicho
wanachokifanya, Manji amesema kuwa ikiwa TFF haitatoa majibu ya kueleweka kwao
ndani ya siku saba, basi moja kwa moja watatua katika Shirikisho la Soka la
Afrika (Caf), ikiwa pia hapo hakutaeleweka ndani ya siku saba, basi wataelekea
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa ajili ya suala hilo.
Manji alionekana kutokuwa na utani kwenye kauli
zake, alionekana kukerwa na kitendo cha Okwi kutua Simba na kusema kuwa Yanga
imevunja mkataba wake, ndiyo maana ameamua kwenda kuichezea Simba.
Waipa siku saba TFF
“Tumepeleka barua TFF, leo (Ijumaa) asubuhi
kutoa malalamiko kuhusiana na Simba kumsainisha Okwi wakijua wazi kuwa ana
mkataba na sisi wa miaka miwili.
“Hii ni barua yetu ya tatu baada ya mbili
tulizopeleka mwezi wa tano na wa saba juu ya malalamiko kwa Okwi kutoitumikia
Yanga kutofanyiwa kazi.
Kutinga Fifa
“Tumetoa siku saba kwa TFF kulitolea ufafanuzi
suala hili na kutoa maamuzi juu ya kilichofanyika na iwapo maamuzi hayatatolewa
ndani ya muda huo, tunatarajia kuwasilisha malalamiko yetu Fifa na ikishindikana
tutaliwasilisha katika Mahakama ya Michezo nchini Uswisi (CAS).
Simba hawajui sheria
za soka
“Viongozi wa Simba wameshindwa kufanya suala la
uungwana kwa kufuata sheria za mpira kama zinavyoeleweka, wangekuja kuwauliza
kwani hatukatai kuuza wachezaji ila sheria ifuatwe.
“Mfano mzuri kina Frank Domayo na Didier
Kavumbagu wamesajiliwa, hatujalalamika kwa kuwa walifuata utaratibu unaotakiwa.
“Upande wangu naona ni jambo la kawaida
kushirikiana, hata mimi nilimpongeza (Evans) Aveva alipochaguliwa kuwa rais
kwani ndiyo mambo ya mpira yalivyo.
Waongeza dau la fidia
“Dau la awali kabla ya kusaini Simba tulitaka
alipe fidia ya dola 200,000 (Sh milioni 320) lakini baada ya kuamka leo
tumeongeza dola 500,000 (Sh milioni 800), kwa hiyo jumla ni dola 700,000 (Sh
bilioni 1.12). Hii tutawadai Simba na Okwi mwenyewe.
Wataka Okwi afungiwe
maisha
“Tumepeleka malalamiko TFF ikiwezekana mchezaji
huyo afungiwe maisha, pamoja na wakala wake kutoshiriki masuala ya soka hapa
Tanzania kutokana na ukiukwaji wa sheria alioufanya ikiwa ni wazi kuwa bado ana
mkataba na klabu yake ya awali.
Apendekeza Simba
ishushwe daraja
“Kutokana na kitendo walichokifanya Simba wasinione
mbaya iwapo timu itashushwa daraja kutokana na kumsajili mchezaji aliyekuwa na
mkataba kwa kutofuata sheria, iwapo walikuwa wanahitaji kumnunua wangekuja na
kuzungumza nasi.
“Kwani sisi huwa tunaachana vizuri na wachezaji
wetu, mfano mzuri Fred Mbuna na Shadrack Nsajigwa ambaye kwa sasa amerudi kuja
kufundisha Yanga, hii ni kutokana na kuachana vizuri.
Atishia kuinunua
Simba
“Mimi nina uwezo wa kununua wachezaji wote wa
Simba na nikawalipa mshahara na jambo hilo naliweza, ila tunachoangalia ni
kufuata kanuni na sheria za soka.
“Kwani hata sisi tungeweza kumchukua (Amissi)
Tambwe kutokana na kumuona ni mchezaji mzuri na kumsajili Yanga lakini hatuwezi
kufanya hivyo kwa kuwa tunatambua sheria na mchezaji huyo ana mkataba ambao
tunauheshimu.
“Hata hivyo Klabu ya Yanga ina mfuko mrefu
kuliko Simba.
Jina lake limo katika
usajili TFF
“Tumewasilisha majina sita ya wachezaji wa
kimataifa akiwemo Okwi kwa kuwa hatukupata majibu yetu mapema kutoka TFF.
“Iwapo wangetupatia taarifa mapema tungeamua
kumuacha mchezaji mmoja, hata Jaja na kumwambia akakae kwa miezi sita kisha
angerudi tena kucheza.
“Siyo kwamba tunalalamika kuwa tunamhitaji
mchezaji huyo kwani kuna wachezaji wengi na tunaweza kwenda kusajili sehemu
mbalimbali duniani ila tunataka sheria ifuatwe.
Okwi ataka kukutana
na Manji
“Okwi alikuja ofisi kwangu na kutaka kuonana na
mimi lakini nikawa bize akaambiwa na katibu muhtasi wangu kuwa atapangiwa siku,
kweli akapangiwa siku, hakutokea, akapigiwa simu hakupokea lakini alitumiwa
meseji hakuweza kujibu wala kutokea tena.
Akana kuvunja mkataba
“Hatujawahi kuvunja mikataba na wachezaji wa
Simba, kwani hata Juma Kaseja tulisubiri mkataba uishe ndiyo tukaingia naye
mkataba…
“…Ndiyo maana tulimsajili pia Kelvin Yondani
baada ya mkataba wake kumalizika, hatukuvunja sheria.
Waunda kamati ya
sheria
“Kesho (leo) tunatarajia kutangaza kamati yetu
mpya ya sheria ambapo ilikuwa ni mpango wa muda mrefu, kwani tumeona ni muhimu
kuwa na kamati hii na isifikiriwe kuwa imetokana na suala la Okwi,” alisema
Manji.
0 COMMENTS:
Post a Comment