RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI. |
SHIRIKISHO la Soka Tanzania
(TFF) linazidi kujaza vituko na mwendo linaokwenda nao sasa linageuka na kuwa
mambo mengi yanayoshangaza, yanayochekesha na yanayoashiria kuwa maendeleo
kwenye mpira yatazidi kuwa ndoto.
Wako wataona TFF
inasakamwa, lakini si watu wa kuhofiwa kwa kuwa ni hisia zao, acha waamini
wanachokiamini, ukweli utafanya kazi yake hata kama itachelewa kuthibitika.
Unakumbuka wakati wa
usajili wa msimu huu wa 2014-15, TFF iliamua kuunda kamati ya uchunguzi wa
kiungo wa zamani ya Yanga, Frank Domayo ambaye alisajiliwa akiwa kwenye kambi
ya timu ya taifa jijini Mbeya.
TFF ilitangaza kupinga
wachezaji kufanya usajili wakati wakiwa kwenye kambi ya taifa. Yanga wakalaumu
kuhusiana na hilo na TFF ikatangaza kuunda kamati ambayo ingetoa majibu juu ya
hilo.
Leo ni zaidi ya miezi
miwili, kimya, hakuna lolote jipya na TFF imekaa kimya huku Domayo akiendelea
kucheza.
Lengo langu si Domayo
azuiwe kucheza Azam FC, au ionekane kuna tatizo. Ninachosisitiza hapa ni majibu
ya suala lenyewe, kwamba TFF ilipaswa kulifanyia kazi na kuweka mambo wazi
kwamba hakukuwa na tatizo au lilikuwepo. Majibu yalikuwa ni lazima kwa kuwa
jambo lenyewe lilitangazwa hadharani na watu wanaendelea kusubiri.
Ukimya wa TFF hadi sasa,
maana yake kuzungumzia suala la kamati ilikuwa ni kutaka kuwapoza wapenda soka
kwa mgongo wa chupa, kumbe hakuna lolote. Sasa TFF imetangaza kuunda kamati ya
kuhujumiwa kwa Taifa Stars.
TFF inaamini Taifa Stars
imetolewa kwenye michuano ya kuwania kucheza Kombe la Mataifa Afrika baada ya
kuhujumiwa! Hivyo imeunda kamati ambayo itachunguza, nasikia kuna vigogo
watahojiwa.
Msisitizo wangu hapa ni
mambo mawili, kwanza ni kwa kamati yenyewe ni lazima isiwe kamati bubu ambayo
inatangazwa tu halafu baada ya muda inapotea na hakuna chochote kinaelezwa.
Kwa kuwa kamati imetangazwa
hadharani kama ile ya Domayo, basi vizuri majibu yake pia yatoke hadharani
ingawa hata wakati inatangazwa, hakukuwa na ufafanuzi wa kutosha kwa nini Stars
ilihujumiwa.
Kwamba TFF waliona kikosi kilikuwa
katika hali nzuri sana, hivyo kuondolewa na Msumbiji ilikuwa ni hujuma? Iko
haja ya kutafakari hilo sana.
Kitu cha pili, mimi naona
hiyo kamati ya Taifa Stars ni kutaka kupoteza muda, fedha na mipango mingine ya
shirikisho hilo kutaka kuwapotezea muda.
Pia ninaona kamati hiyo
inatengenezwa kwa lengo la kutaka kuwakomoa baadhi ya watu au kuwachafua tu
kupitia kigezo hicho. Ambacho ninaweza kusema, TFF ina kila sababu ya kufanya
juhudi katika soka la vijana.
Fedha ambazo zitatumika
kwenye kamati hiyo, nguvu itakayotumika kuunda kamati, kuwasiliana na hata
kukaa kwa ajili ya kuwahoji watu, ingeelekezwa kwa vijana ambao watalisaidia
taifa letu hapo baadaye.
Taifa Stars tuliona
ikicheza kwa kiwango kizuri katika kipindi cha kwanza dhidi ya Msumbiji, ilikuwa
angalau. Kipindi cha pili ikazidiwa kabisa, hakuna asiyekumbuka hilo.
Sasa kama kulikuwa na
hujuma, basi ianzie kwa kocha, wachezaji na TFF yenyewe kwamba Watanzania
tulikuwa nyuma ya timu kwa kila hali, lakini ikashindikana na ilikuwa vigumu
kuingia kuwasaidia.
Siamini kama kamati hiyo
pia itakuwa ni sehemu ya TFF kuendelea kutaka kupoza mambo kwamba inaonewa,
inahujumiwa na kuwaambia Watanzania kuna kamati imeundwa ili kupoza mambo na
kuwasahaulisha machungu yao dhidi ya madudu ya TFF na sasa timu ya taifa.
kaka kweli kabisa nakubaliana na hoja zako, kiukweli hata mimi sielewi TFF wanafanya nini kwan zaid hawafikirii kuhusu kukwamua soka letu na zaid ni propaganda tu. Naamini sasa mpira wetu ni siasa tu,na tusitarajie maendeleo ya soka letu.
ReplyDeleteNini kifanyike:-
1. Siasa za Usimba na Uyanga zife
2. Viongozi wengi wa TFF ni washabiki wa mpira na si wapenzi wa mpira.
3.Kuwe na mpango mkakati na ufuatiliwe.
4. Kuepushwa viongozi maslah na wapewe viongozi wapenda soka/mpira na si viongozi wanao zipenda Simba na Yanga