Na Saleh Ally
NILISHIRIKI
kwenye programu maalum ya Didier Drogba kwa ajili ya kuwahamasisha vijana raia
wa Ivory Coast kutamani kupata mafanikio makubwa kupitia uhamasishaji wa nyota
huyo.
Nikashuhudia
programu nyingine na Victor Wanyama, nahodha wa timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee
Stars’ akiwahamasisha watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, kwamba siku
moja nao wanaweza kuwa wachezaji bora tegemeo wa Kenya ambao wanacheza soka la
kulipwa na kupata mishahara mikubwa.
Programu
hizo mbili za Abidjan na Nairobi, zimekuwa zikinifanya nikumbuke nyumbani mara
kadhaa, kwamba Tanzania tunaweza kufanya hivyo kupitia nani? Kweli tuna
wanamichezo wengi lakini wako wanaoweza kuwa msaada zaidi.
Hasheem
Thabeet Manka ndiye mwanamichezo maarufu zaidi kwa hapa nyumbani. Anacheza ligi
kubwa zaidi kwa maana ya kiwango, ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza
kucheza Ligi ya Kikapu Marekani (NBA).
Thabeet
analipwa zaidi ya dola milioni 1 (zaidi ya Sh bilioni 1.6) kwa mwaka. Pia ni mwanamichezo
ambaye karibu kila siku ya uhai wake anaitangaza Tanzania kwa kuwa wengi
wangependa kujua kuhusu yeye na nchi gani anayotokea.
Ndiyo
maana hata baada ya Rais Barack Obama wa Marekani kufanya ziara nchini,
alimtaja Thabeet kwamba ana habari zake kwa kuwa amecheza kwenye timu za NBA.
Marekani
ina watu zaidi ya milioni 300, jiulize vijana wangapi wangependa kuwa nyota wa
mpira wa kikapu, wangapi wana ndoto ya kucheza NBA? Wengi sana lakini
wameshindwa na Thabeet ambaye katokea nchi ambayo mchezo huo hata haupewi
kipaumbele.
Nani
anawaza kuhusu kumtumia Thabeet kwa ajili ya kuhamasisha watoto, vijana na
wengine wenye malengo ya kufanikiwa? Ni mwanamichezo huyo pekee ambaye utaona
amefika mbali kuliko wengine wote nchini, lakini zaidi kwa juhudi zake binafsi.
Utaona
asilimia kubwa ya wanamichezo au wadau wa soka wamekuwa wakitumia muda mwingi
kumlaumu Thabeet, kwamba hapati nafasi ya kucheza au vinginevyo. Lakini
wanajisahau au hawajui kuhusiana na alifikaje hapo.
Wakati
anapita kwenye draft ambayo inahusisha wachezaji zaidi ya 500, Thabeet alishika
nafasi ya pili kwa ubora. Wanaokuwa katika nafasi za juu 20 wanakuwa na kiwango
cha kucheza NBA.
Wapo
wanaosema kwamba Thabeet anaendekeza starehe, ndiyo maana hapati nafasi ya
kucheza, hawajiulizi maswali ya msingi, kwamba ushindani anaokutana nao ni wa
kiasi gani. Mfano Oklahoma City Thunder alikuwa anacheza na wachezaji kama
Kevin Durant na wengine.
Wamarekani
au wale wanaotokea nchi za Ulaya, wamecheza mpira wa kikapu miaka nenda rudi.
Wamekuwa kwenye shule zinazoshiriki mchezo huo, usisahau wamehamasishwa na
wachezaji wengi nyota kama Earvin ‘Magic’ Johnson, Michael Jordan na wengine
wengi.
Thabeet
amesomea shule ipi yenye kiwango kizuri au cha juu cha mpira wa kikapu? Au nani
alimhamasisha kufikia hapo alipo? Maana amewapita Watanzania wote kufikia
kiwango hicho!
Yako
ya kujifikiria na kumpongeza. Simaanishi asikosolewe, lakini si vema kumkatisha
tamaa na asingekuwa na lolote timu ya 76eras iliyomnunua kutoka Oklahoma City
Thunder isingekubali kutoa zaidi ya dola milioni 1 ili kuipata huduma yake.
Ndiyo
maana nasisitiza kuwa, tuna bahati ya kuwa na Thabeet, inawezekana ni zawadi
kutoka kwa Mungu lakini hatuitumii. Nani anafanya programu za kuinua na
kuendeleza vijana, kumpa nafasi awasaidie vijana kuhamasika kwamba inawezekana?
Thabeet ni mtoto wa maskini tu, marehemu Thabit
Manka. Msomi aliyeilea familia yake kwa makuzi mazuri akishirikiana kwa kila
hali na mkewe. Inawezekana hiyo imemsaidia Thabeet kufika alipo sasa.
Hapa
naiona faida ya Thabeet mara mbili, kwanza nguvu ya malezi aliyopata, lakini
nguvu ya maneno na mafunzo anayoweza kuyatoa kupitia njia alizopita, ugumu
ulivyokuwa, kutovunjika kwake moyo na hadi kufikia yalipoanza kuonekana
mafanikio na baadaye kupatikana.
Serikali
inafanya nini kupitia wizara husika kumshawishi Thabeet kufanya programu maalum
kama zile za kina Drogba na Wanyama? Nini kinashindikana hapo?
Ninaamini
Thabeet angekuwa Mkenya au kutoka
Ivory Coast wala wasingelala kama ilivyo kwetu Tanzania ambao kila kitu tunaona
rahisi tu huku lawama zikiwa nyingi hata kwa wale ambao hawajafanikiwa na
lolote.
Wakati
mwingine naamini ni roho mbaya au wako wanaoamini kufanya hivyo kutachangia Thabeet ajulikane zaidi. Lakini tunapoteza
bahati kubwa ya kuwasaidia watoto na vijana wetu.
Tusimuache
Thabeet kila akirudi nyumbani likizo, eti ajitolee yeye mwenyewe kuwafundisha
vijana. Liandaliwe fungu maalum ikiwezekana atembee hadi mikoani ili
kuwahamasisha vijana walio tayari kucheza mpira wa kikapu lakini bado wanaamini
haiwezekani na huenda alipofika yeye ni bahati nasibu au alitakiwa kufika yeye
tu na hakutakuwa na mwingine.
Najua
mambo ya serikalini ni kama kobe, watu wengi si wabunifu na wanaona sawa
kufanya mambo kupitia utaratibu wa kawaida na ikaonekana poa tu. Lakini huu
ndiyo wakati mwafaka wa kubadilika.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment