September 12, 2014



NAWEZA kutofautiana na watu wote katika suala la kugombewa kwa mshambuliaji Emmanuel Okwi, lakini nitaendelea kusisitiza hivi, suala hili linaongozwa kishabiki sana badala ya utaalamu.


Sifa ya binadamu mwema, kwanza kabisa ni kuwa mkweli, ndiyo kitu kitakachokuongoza kwenda kwenye mambo mengine mema. Uoga ni utumwa, achana nao.

Funga macho yako mawili, vuta pumzi na kuitoa halafu anza kutafakari kama kweli Yanga na Simba zinapaswa kutumia nguvu nyingi kiasi hicho kumgombea Okwi? Utapata jibu, tukikutana, tutajadiliana.

Kabla ya kukutana acha nikueleze ninachoamini kwamba, Yanga na Simba zinaongozwa na ushabiki ambao hauna manufaa. Kwa kuwa zingeweza kufanya mambo mengi ya msingi kuliko kumgombea Okwi.

Inawezekana huu ulikuwa ni wakati mwafaka wa Yanga kuonyesha wazi kuwa unadai nini hasa kwa Okwi, kama kweli barua yao imeonyesha walitaka kuvunja mkataba, Okwi amewarahisishia kuuvunja huo mkataba.

Jiulize Yanga wanapaswa kumdai Okwi sasa, wa nini kama walitaka kuvunja naye mkataba. Kama wana madai mengine, basi hayo wayashikilie na ndiyo maana nasema, kama ni kesi ya Kamati ya Sheria ya Hadhi za Wachezaji ya TFF kumruhusu kucheza Simba, hilo halipaswi kuiumiza Yanga.

Tokea mwanzo, ilionyesha haina shida naye. Hivyo sasa ni wakati wa kulilia stahiki nyingine mfano madai ya fedha, lakini si kupambana eti hawezi kucheza Simba. Mfano akibakizwa Yanga, je, itakuwa tayari kumtumia?

Katika hali ya kawaida jibu ni hapana na inaonyesha wazi kwamba haimtaki, sasa kwa nini iendelee kupambana kumpata? Ndiyo kichekesho cha kwanza.

Kwa Simba, bado kuna hali ileile ya kuchekesha. Kama unakumbuka Okwi aliuzwa kwa Etoile du Sahel ya Tunisia kwa dola 300,000 (Sh milioni 480), lakini kabla ya hapo ilimlipa dola 40,000 ambazo zilipotea bure.

Hadi leo Simba haijalipwa fedha zake na ina kesi ya madai kuhusiana na mchezaji huyo. Inajulikana hakukuwa na uamuzi uliopitishwa Okwi kufikia kuichezea Yanga, mwisho ikaonekana inafaa.

Sasa Simba nayo imeingia tena kwenye mkumbo huo wa Okwi, hii ni kuonyesha kwamba imekubali kuzipoteza fedha zile dola 300,000. Yaani imenyoosha mikono haiwezi kuzipata?

Kama Simba itakuwa inazihitaji fedha hizo, bado Etoile nayo inaweza kuwa na sababu ya uhakika sasa kutoilipa Simba hata senti kwa kuwa mchezaji inayetaka ilipwe, tayari yuko Msimbazi tena.

Kama Simba bado inataka ilipwe, kuwa na Okwi tena haioni ni kupoteza fedha hizo au kujiwekea ugumu zaidi? Na kama imeamua kuzisamehe, je, Okwi wa sasa ana thamani ya fedha hizo milioni 480?

Ndiyo maana naona mchezo huu wa Okwi umetawaliwa sana na ushabiki, mfano Simba kuonyesha imelipa kisasi baada ya Yanga kumchukua Okwi wakati wenyewe wakiendelea kuidai Etoile.

Lakini Yanga nayo iko tayari kupoteza fedha zaidi ili iweze kuionyesha Simba ambaye ni mtani wake kwamba inaweza zaidi yake. Unajua watu wanaoshindana wanavyopenda kushindana bila sababu za msingi, ndivyo wanavyofanya watani hawa.

Vizuri kujitambua, vizuri kujiamini na mwisho kuamua kitu ambacho ni sahihi kwa maslahi ya klabu, si kwa maslahi ya kuwafaidisha mashabiki au wanachama kitu ambacho kimekuwa kikichangia kwa muda mwingi viongozi kufanya maamuzi ambayo si sahihi.

Viongozi wengi wamekuwa wanafanya maamuzi yanayolenga kuwaonyesha mashabiki na wanachama. Kweli Yanga ina haki ya kudai stahiki zake kwa kuwa Okwi alikuwa na makosa, lakini ni sahihi kumpigania asicheze Simba? Simba nao wana sababu ipi ya kuona Okwi ni muhimi sana? Hawataki fedha zao dola 300,000? Wakimchukua hawaoni wanaua nguvu ya kesi hiyo? Je, hawakuwa na nafasi ya kupata mchezaji mwingine mwenye uwezo hata zaidi ya Okwi? Shidaaaa.


5 COMMENTS:

  1. Napenda kusema machache tu. Kuhusu Yanga kumdai Okwi haiwezi kuwa sahihi kwa sababu hawakutekeleza matakwa ya kimkataba yaliyosababisha mchezaji kukimbia, mfano rahisi ni huu ufuatao. Ikiwa abiria kapanda basi kutoka Dar kwenda Arusha na hakulipa nauli kufika Chalinze gari likaanza kusumbua na kuhatarisha safari, akishuka kondakta atathubutu kumdai nauli? Kuhusu Simba kukosa pesa za Okwi pia sio sahihi kwa sababu kama Simba wangemchukua Okwi moja kwa moja wakati akiwa na mgogoro na Otoel du Sahel wangepoteza haki kwa sababu Etoel wangeweza kujenga hoja kwamba Simba ndio waliomshawishi, lakini kwa mazingira ya sasa ambayo mchezaji kaidhinishwa kucheza vilabu tofauti viwili hadi kufikia kuidhinishwa Simba kama kilabu cha tatu hakutaathiri madai yao.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Huwezibkushindwa kulipa nauli kabisa, utalipia hadi hapo ulipofika baada ya hapo utaamua kutafuta gar nyingine ambayo unahisi kwako j salama zaidi huwezi shindwa kulipa hata kidogo

      Delete
  2. Ukiwa mchambuzi au muandika makala, pamoja na kuwa ni maoni yako na una haki ya kuyatoa, mimi naamini ni lazima uwe unafikiria hatua moja au zaidi mbele kuliko mtu mwingine wa kawaida. Nadhani kuhusu Yanga ni kweli hata mimi sidhani kama walimuhitaji kwa dhati, walishamchoka na hata kwenye usajili walimkata, lakini kwenye hili la Simba kuwa watapoteza haki yao toka etoile du sahel kisa kumsajili tena Okwi ni hoja nyepesi sana na hukuifikiria vizuri hata kidogo. Havihusiani hata kidogo, okwi hajarudi simba kutokea etoile du sahel. Ameshapita vilabu vingine tena kwa kuuzwa (toka villa kwenda Yanga). Na ameenda Simba toka Yanga, INAHUSIANA VIPI na Etoile kutolipa deni la Simba. Etoile wanaweza wasilipe deni kwa hoja zao nyingine kabisa, lakini wakileta hoja kama hii yako watachekwa na dunia nzima na kesi itakuwa rahisi sana. Fikiria upya...

    ReplyDelete
  3. Kwa kifupi Umechemka mno kwenye hoja ya Simba na deni lao la dola 300,000. Hakuna uhusiano kabisa wa deni hilo na usajili huu wa okwi

    ReplyDelete
  4. Saleh akili ya Hans pope changanya na yakwako!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic