Na Saleh Ally
WATANZANIA ni watu wacheshi na kwenye michezo inaweza
kuwa sehemu ya kuhakikisha namna wanavyowapokea wachezaji au makocha wageni.
Furaha na ukaribu unatangulia hata kabla ya kuanza
kufanya kazi, lakini hawana muda wa kupindisha maneno inapofikia wamechoshwa,
hasa kwa waliyemuamini, halafu akawaangusha.
Makocha na wachezaji wa kigeni ambao wamejiunga na timu
za Yanga, Simba na nyingine kwa ajili ya msimu ujao wana madeni makubwa ya
kuonyesha furaha ya mashabiki hao ilikuwa sahihi.
Lazima wafanye vema kuziokoa timu hizo ambazo zinawalipa
vizuri, zimeonyesha kuwajali. Tena mashabiki wakaonyesha heshima na upendo wa
juu. Inawezekana wako wengi lakini hawa ni sehemu yao na wanapaswa kulishikilia
suala la deni wanalotakiwa kulipa.
Marcio Maximo:
Anapata mshahara wa dola 12,000 (zaidi ya Sh milioni 19)
kwa mwezi. Nyumba nzuri na usafiri ni Toyota Prado, inawezekana kabisa
hakutakuwa na sababu ya kusema kazi yake ina mushkeli.
Maana yake anatakiwa kuipa Yanga mafanikio na muhimu
kwake ni ushindi na kurejesha heshima ya juu ya klabu hiyo ambayo ndiyo imeanza
kujipanga upya kwa gharama nyingi kuhakikisha inarejesha ubingwa.
Hana sababu ya kuwa na visingizio kibao kwa kuwa
mazingira ya soka ya Tanzania anayajua vizuri ingawa kwa mara ya kwanza ataanza
kukumbana na changamoto ya viwanja vya mikoani ambavyo hakuwahi kwenda kwa kuwa
alikuwa ‘mvivu’ kutembelea mikoani kusaka vipaji alipokuwa kwenye kikosi cha
Taifa Stars.
Patrick Phiri:
Kweli ni mzalendo na ana mapenzi ya dhati kwa Simba,
angalia ameikimbia kazi ya kuinoa timu ya taifa ya Namibia ambayo ingekuwa na
maslahi makubwa kwake, amekubali kurejea Msimbazi.
Mshahara wake si mnono wa kutisha, dola 5,000 (Sh
milioni 11), Simba wamempokea kwa shangwe kwa kuwa wanaijua kazi yake, kweli ni
kocha bora, hilo halina ubishi.
Ukweli unabaki palepale, historia haiamui wakati uliopo.
Lazima afanye vizuri sasa na tayari ameonyesha matunda kwenye mechi za kirafiki
lakini hakuna ubishi, majibu ni kwenye ligi. Simba wanataka kurudisha heshima yao,
miaka mitatu sasa, ‘full’ mateso.
Leonardo Leiva:
Akiwa mazoezini ameonyesha ni mtu anayeipenda kazi yake,
juhudi za juu. Kweli ni kocha anayetaka kuona kikosi chake kinafanikiwa. Achana
na mshahara mzuri na makazi bora eneo la Masaki alilopewa na Yanga, lakini
usafiri na kila anachohitaji, anapata.
Sasa wakati wa kuilipa Yanga ndiyo huu, mechi za ligi na
zile za kirafiki. Ajue iwapo akishindwa, siku mzigo ukimuangukia bosi wake,
naye atakuwemo.
Jaja & Coutinho:
Hakuna hadithi siku hizi, Geilson Santos Santana ‘Jaja’ na
Andrey Coutinho kila mmoja ameonyesha uwezo wake katika mechi za kirafiki na
kufunga mabao mawili katika mechi walizocheza.
Kwa maana ya wachezaji wanaoweza kuisaidia Yanga,
inaonyesha ndiyo. Majibu sahihi yanatakiwa katika mechi za ligi na zile za
kimataifa, zile za kirafiki zilikuwa ni pasha moto tu.
Hivyo, Jaja na Coutinho wana deni kwa kuwa mshahara wa
dola 2,000 (Sh milioni 3.6) kila mmoja, nyumba nzuri ya kuishi na hakuna ubishi
ni wachezaji wa kulipwa ambao wanategemewa, lazima kuwe na mafanikio.
Paul Kiongera:
Katokea KCB Kenya akiwa mmoja wa washambuliaji tishio,
bado Paul Modo Kiongera ameonyesha kuwa ni hatari, kwani mechi mbili za
kirafiki na Simba amefunga mabao mawili.
Kazi yake imemridhisha kila mtu. Kikubwa akumbuke
amecheza vizuri kwenye trela ila muvi ndiyo linaanza, Ligi Kuu Bara. Hakuna
ujanja wala hadithi, lazima afanye vizuri hapo.
Kufunga ndiyo, kutengeneza pasi zinazozaa mabao ndiyo zaidi.
Hivyo lazima Simba iwe bingwa au kushika nafasi ya pili, la sivyo mengine
yatabaki hadithi isiyokuwa na mwisho mzuri.
Pierre Kwizera:
Mrundi huyu Simba wanaweza wasiwe na hofu hata punde,
licha ya kwamba hakupokewa kwa mbwembwe, lakini ni kiungo hasa ambaye
atashangaza kwa pasi zake za uhakika.
Anajiamini, mtulivu, anaijua kazi yake. Ameonyesha
kwenye mechi chache za kirafiki, lakini bado hiyo ni trela, muvi ni Ligi Kuu
Bara.
Pasi na kujiamini kwake ndiyo kutakuwa malipo kwa Simba
kuthibitisha mengi likiwemo lile la kuchaguliwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya
Ivory Coast wakati akiichezea Afad.
0 COMMENTS:
Post a Comment