OKWI WAKATI AKIWA YANGA |
Aliyekuwa Kocha wa Simba, Abdallah
Kibadeni, amefunguka kuwa tatizo linalomtesa mshambuliaji wa Simba, Mganda,
Emmanuel Okwi kiasi cha kushindwa kuonyesha kiwango kama zamani ni kutokana na madeni
ya Yanga yanayomkabili.
Okwi aliyesajiliwa Simba hivi karibuni
akitokea Yanga, amekuwa na vuta nikuvute na viongozi wa klabu hiyo ambayo
inamdai fedha nyingi kutokana na kutoichezea timu hiyo ipasavyo msimu uliopita
ikiwa ni pamoja na kuondoka.
Yanga ilipeleka malalamiko yake Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), ikimdai Okwi kiasi cha dola 200,000 (Sh milioni 333) kama
fidia ikiwa ni fedha za mishahara waliyokuwa wakimlipa na fidia ambapo hadi
sasa kumekuwa na hali ya vuta nikuvute kutokana na kuliwasilisha suala hilo
Fifa.
KIBADENI (KUSHOTO) WAKATI AKIWA SIMBA. |
Hata hivyo, licha ya hayo yote kutokea,
mchezaji huyo hajafumania nyavu hata mara moja tangu atue Simba katika timu
hiyo kuanzia mechi za kirafiki hadi ile ya ligi kuu dhidi ya Coastal Union,
zaidi ya kutoa pasi ya bao kwa Amissi Tambwe.
Kibadeni
amefunguka kuwa, kitu ambacho kinachangia kwa kiasi kikubwa kumfanya Okwi
ashindwe kucheza katika kiwango chake kilichozoeleka ni pamoja na madeni
anayodaiwa na Yanga na ndiyo yanayomfanya ashindwe kuwa vizuri.
“Unajua kitu kinachochangia Okwi kutokuwa
katika kiwango kizuri ni hali ya madeni inayomuandama kwani kila kukicha
hutokea jambo hili mara lile, hivyo inamsababisha mchezaji kuwa na msongo wa
mawazo na kushindwa kufanya vizuri.
“Kiwango chake cha sasa kimeshuka tofauti na
ilivyokuwa awali, nadhani hii imetokana na kudaiwa na timu mbalimbali,
anahitaji kutulia kwa kutofikiria mambo yanayomkabili ili aweze kurudi katika
hali yake ya zamani kwani alikuwa mchezaji hatari.
“Nadhani hali hii ikimalizika na kutulia
kabisa na kupata mtu sahihi wa kumchezesha, basi atakuwa vizuri kwa kurudisha
kiwango chake,” alisema Kibadeni.
Hata hivyo, Okwi amefungua kesi ya kuidai
Yanga zaidi ya shilingi milioni 111 ikiwa ni fedha iliyobaki ya usajili pamoja
na kodi ya nyumba chini ya mwanasheria wake, Damas Ndumbaro.
0 COMMENTS:
Post a Comment