SIMBA |
MECHI za raundi ya pili ya Ligi Kuu Bara,
zinatarajiwa kuchezwa leo na kesho Jumapili kwenye viwanja tofauti.
Leo Jumamosi kutakuwa na mechi tano, Simba
ambayo inanolewa na kocha Mzambia, Patrick Phiri, itakuwa kwenye Uwanja wa
Taifa ikiwakabili maafande wa Polisi Moro.
Yanga inayonolewa na Mbrazili, Marcio Maximo,
itashuka dimbani kesho Jumapili kuvaana na Tanzania Prisons ya jijini Mbeya
huku ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar, hivyo itakaza
kuhakikisha inapata ushindi wa kwanza kwenye uwanja wa nyumbani.
Prisons ambayo katika mchezo wake wa kwanza
iliichapa Ruvu mabao 2-0, inakumbukumbu ya kuchapwa mabao 5-0 kwenye mchezo wa
mwisho waliokutana na Yanga msimu uliopita, hivyo imepanga kufuta uteja.
Aidha, kwa upande wa Simba ambayo ilitoka na
sare ya mabao 2-2 na Coastal Union ya Tanga, itakuwa na kibarua kigumu leo
katika Dimba la Taifa kutokana na wapinzani wao Polisi Moro ambayo imepanda
daraja msimu huu kuhitaji kushinda katika mchezo huo kufuatia kufungwa mabao
3-1 na Azam FC katika mchezo wa kwanza.
Hata hivyo, Simba itakuwa na wakati mgumu
kufuatia baadhi ya wachezaji wake tegemeo, Paul Kiongera, Ivo Mapunda, Miraji
Adam na Jonas Mkude kutocheza mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi.
Kwa upande wa Azam, yenyewe itakuwa na kazi
kubwa ya kuhakikisha inaendelea kutetea ubingwa wake ilioupata msimu uliopita
kwa kufanikiwa kuendeleza wimbi la ushindi dhidi ya Ruvu Shooting ambayo
iliifunga mabao 3-0 msimu uliopita ambapo watakutana katika Dimba la Chamazi
nje kidogo ya Jiji la Dar ambapo wanatarajiwa kukutana na upinzani mkubwa kutokana
na wapinzani wao kufungwa mabao 2-0 katika mchezo wa awali.
Mechi nyingine ambazo zitacheza leo ni: Mtibwa
Sugar Vs Ndanda, Uwanja wa Manungu, Morogoro, Mbeya City Vs Coastal Union,
Sokoine, mechi za kesho itakuwa ni JKT Ruvu dhidi ya Kagera Sugar, Azam Complex
na Yanga Vs Prisons.
Msimu uliopita mabingwa walikuwa Azam FC ambao
waliibuka na pointi 62, nafasi ya pili ilishikwa na Yanga iliyomaliza na pointi
56, Mbeya City iliyoshika nafasi ya tatu, ilipata pointi 49 na Simba iliyoshika
nafasi ya nne ilijikusanyia pointi 38.
0 COMMENTS:
Post a Comment