KATIKA suala la idadi ya
mashabiki hapa nchini ukizitoa Simba na Yanga, inafuata Mbeya City, hili
linajidhihirisha pale inapotokea timu hiyo inapambana uwanjani na timu nyingine,
utaona umati wa watu walio nyuma ya timu hiyo ukiutaka ushindi kwa udi na
uvumba.
Mashabiki wa City ambayo
ilipanda ligi kuu msimu uliopita na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu,
wanasifika kwa uzalendo mkubwa walionao kuhusu timu yao katika kuungana kwa
pamoja kuisapoti timu ya mkoa wao, hili limekuwa likiwapa faraja hata viongozi
wa timu hiyo na kuwaweka kama moja ya chachu za ushindi wa timu hiyo.
Lakini pamoja na hayo, mashabiki
hao tayari wametengeneza matawi yao ya ushangiliaji pamoja na mikakati mingine
ya kuisaidia timu kwa namna moja au nyingine katika kuhakikisha inapata
mafanikio zaidi.
Mbali na hayo, mashabiki
hao pia wanazungumzia mengi kuhusiana na timu yao hiyo ikiwemo furaha, hofu na
hata presha wanayoipata kutokana na timu yao.
Championi Jumatano lilizungumza
na baadhi ya mashabiki wa Tawi la Wakali wa Donta, lililopo maeneo ya Uhindini
mkoani hapa ambapo Bernard Guga na Kelvin Mkwaza, waliwawakilisha wenzao wa
tawi hilo na kuzungumza yafuatayo:
Mbeya City ndiyo faraja
pekee ya soka mkoani hapo
“Yaani kabla haijaja hii
Mbeya City, sisi wakazi wa hapa tulikuwa hatuna timu ya kushangilia kwa sababu
Prisons ilikuwa imetutenga kwa hiyo tukawa tupotupo tu, tukawa tunasubiri timu
za Dar zikija ndiyo tunamaliza kiu yetu ya kushangilia soka.
“Lakini tangu kuanzishwa
kwa Mbeya City sasa tuna amani sana na tunaona raha ya mpira,” anasema Benard.
Simba, Yanga ndiyo zinatupa
presha ya kufika tunapotaka
“Kama ni soka tu, kwa kweli
huwa tunazihofia hizi timu za Simba, Yanga na Azam, maana zinapiga kweli mpira
na hata ikifika siku tunakutana nazo, basi tunakuwa na hofu kwelikweli, tunajua
leo tunakwenda uwanjani kushangilia ila kazi ipo.
“Lakini muda mwingine huwa
tunazihofia kwenye suala la kununua mechi na vitu kama hivyo, kwa sababu
hutumia ukongwe na pesa zao kujipatia matokeo, ingawa hatuna ushahidi katika
hilo, lakini kuna vitu huwa tunaviona uwanjani vinavyoonyesha kabisa kwamba
hapa mshindi ameshapangwa.
Hatuwezi kuwashangilia
Prisons hata siku moja
“Yaani hawa Prisons sasa
imefika hatua tumewatengea kabisa jukwaa lao, kwa sababu hawafiki hata 20, wanataka
upinzani na sisi halafu hawana mashabiki wa kuweza kushindana na sisi.
“Wakicheza na timu za mikoani sisi huwa tunawazomea wafungwe,
halafu na sisi tukicheza, wao wanakuwa upande wa wapinzani. Kwa hiyo hayo ndiyo
maisha yetu na haitakuja siku tuwashangilie tena kwa sababu walituudhi
walipotutenga mara ya kwanza.
Azam walituudhi sana msimu
uliopita
“Hakuna siku tuliyoumia na
kuudhika kama kwenye mechi ya marudiano na Azam tuliyofungwa 2-1 msimu uliopita.
“Yaani mpira unaendelea lakini unaona kabisa hapa kuna fitna
imefanyika na matokeo yameshapangwa tangu awali, tuliumia sana siku hiyo na tangu
hapo tukaapa kuwa ukiwatoa Prisons wapinzani wetu wengine ni Azam kwenye ligi,”
anamalizia Benard.
Kuondoka kwa kocha ni pigo
kubwa kwetu
“Ngoja nikwambie ukweli
kaka, unajua kuondoka kwa Maka (Mwalwisi, aliyekuwa kocha msaidizi wa Mbeya
City ambaye sasa anaifundisha Panone FC ya Arusha) ni pengo kubwa kwa kweli,
ukiachana na ualimu wake mzuri lakini jamaa alikuwa na uwezo wa kuwaleta pamoja
wachezaji, kuwapanga na kuwatoa hofu ya mechi.
“Yaani hata mchezaji akiwa
mtukutu lakini yeye alikuwa na uwezo wa ‘kumcontrol’ na kumweka sawa na mambo
yakaenda, sidhani kama kuna mtu atakuja kuziba pengo lake,” alisema Machaza.
Kuhusiana na hilo shabiki
mwingine ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema: “Kuondoka kwa Maka ni pigo
kwetu, ingawa hawezi kutusababisha tukafeli msimu huu lakini kwenye pengo kuna
pengo tu.”
Benard akamalizia: “Maka
alikuwa na ufundi wake katika vitu vingi ikiwemo hata kuvumbua vipaji lakini
hata aliyekuja pia tutamwamini na kuangalia kazi yake.”
Tuna hofu kubwa sana msimu
huu
“Sisi matumaini yetu
tunataka tuzidi kusonga mbele zaidi ya hapo tulipo sasa, lakini kwa kuwa ile
ligi haitabiriki basi hata kama tukifanya vibaya, tusitoke kwenye zile nafasi
nne za juu.
“Kuhusu hofu yetu kwa sasa
unajua wengi wameshatujua kwamba sisi ni wazuri na tumeshakuwa moja ya timu
ngumu, kwa hiyo tutakapokutana na timu yeyote ile mechi itakuwa ngumu.”
Akikosekana Yeya, Nonga
tunakuwa hoi
“Sisi tunaipenda timu kwa
ujumla lakini kama ikitokea siku, mmoja kati ya Anthon Matogolo, Mwegane (Yeya)
na Nonga (Paul) anakosekana, basi kidogo tunaingiwa na wasiwasi kwa sababu hawa
wachezaji ni watu wa matokeo muda wowote.”
Vipi kuhusu udhamini wa Bin
Slum
“Kwa kweli kuhusu huu
udhamini mpya tulioupata kutoka kwa Bin Slum kupitia betri zake za RB ni mzuri
na tunaamini kupitia udhamini wake huo, tunaweza kufanya vizuri na kusonga
mbele zaidi,” anasema Makwaza.
0 COMMENTS:
Post a Comment