ISIHAKA. |
Wakati kikosi cha Simba kikitarajia kushuka uwanjani kesho Jumamosi
kupambana na Polisi Moro katika mechi ya Ligi Kuu Bara, beki wa kati wa timu
hiyo, Hassan Isihaka amewaomba msamaha mashabiki wa timu hiyo kutokana na
makosa aliyoyafanya uwanjani Jumapili iliyopita dhidi ya Coastal Union ya
Tanga.
Katika mechi hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam, Isihaka alifanya makosa kadhaa likiwemo lile la kuunawa mpira nje
kidogo ya eneo la 18 ambalo lilikuwa na faida kwa Coastal, kwani ilijipatia bao
kupitia kwa Rama Salim na kufanya matokeo kuwa 2-2.
“Naomba wanisamehe kwa yote yaliotokea katika mechi hiyo na
wasinielewe vibaya kwani sikukusudia kufanya hivyo ila hali hiyo ilitokea kwa
bahati mbaya wakati nikijaribu kuondoa mpira kwenye eneo hilo la hatari,”
alisema Isihaka.
Isihaka ni kati ya mabeki wanaochipukia katika kikosi cha Simba na
wanaonyesha mwendo wa kuja kuwa kati ya wale bora baadaye.
Hata hivyo atatakiwa kujituma ili kuendelea kuimarisha kiwango chake
kwa kuwa soka linabadilika kila kukicha na ushindani unapanda.
0 COMMENTS:
Post a Comment