Na Saleh Ally
USISHANGAZWE nami
kuamua kujaribu kumshawishi aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), Leodegar Chilla Tenga arejee tena ili kusaidia kuyatoa kwenye matope
magurudumu ya shirikisho hilo.
TFF imekwama, rais
wake Jamal Emily Malinzi, amefeli na hali inaonyesha wazi kuwa tuendako kuna
hatari zaidi ya kutumbukia kabisa shimoni.
Kuna mengi ya
kuonyesha kwamba Malinzi amefeli na kwa kuwa watu wanaona haya kuelezana
ukweli, wanachukia kukosolewa, huenda kilichofanywa na TFF ya Tenga kwa mihula
miwili, kitaporomoka na kupotea kabisa ndani ya nusu mhula wa Malinzi,
nitafafanua.
Yamepita mengi
kama ambayo tumeona, ile Taifa Stars maboresho iliyopotelea kusikojulikana na
hakuna faida ya kusema ilikuwa imewekwa kwa malengo zaidi ya kuwasikia viongozi
wakisema kuna wachezaji wa timu hiyo wamesajiliwa timu fulani tena asilimia 5
tu ya wachezaji hao, wengine hawajulikani walipo.
Matumizi mabaya
na kuhama ofisi zao kwenye kupanga kwa mamilioni lukuki ni jambo jingine. Lakini
kufeli kwa Taifa Stars ambayo iliwekewa ahadi kibao na sasa zinaanzishwa kamati
tu eti za kutafuta walioihujumu ikionyesha wazi ni janja ya kutaka kuwaziba
Watanzania macho na masikio.
TFF ya Malinzi ni
ile inayokwenda na mtindo wa ‘unfinished business’. Hakuna ilichokianza,
ikikimaliza na kila ilichofanya kimefeli, huenda kipo, basi watanikumbusha.
Sijui kama kuna
yule anayeweza kukataa kuwa TFF ya sasa imejaa ubabe, inayoangalia itapata vipi
fedha bila ya kujali wengine wataathirika vipi.
Mfano mzuri ni
sakata la TFF sasa kuagiza klabu zianze kukatwa udhamini wao wa Vodacom na Azam
TV ili ziende kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Soka (FDF) eti ina mpango wa
kusaidia vijana.
Ni maajabu saba
kusikia eti kuna watu wanaona TFF iko sawasawa, inajenga hisia katika masuala
yanayotakiwa kufanyiwa kazi kuusaidia mpira wetu, wako wanaofanya ushabiki kwa
kuwa tu wanaweza kusaidiwa kurahisisha maisha yao!
Mpira huu ni kwa
faida ya sisi tuliopo, wadogo na watoto wetu, pia vizazi vijavyo. TFF inafeli
kwa kuwa inataka kuyapeleka mambo kiswahiba, kwa kubahatisha na viongozi
kuangalia watapata nini, si mpira utapata kipi kwa ajili ya leo na baadaye.
Kichekesho cha
kwanza ni kwamba TFF ndiyo inachukua fedha nyingi zaidi kwenye udhamini wa Azam
TV na Vodacom kuliko hata klabu moja, hii ni kwa kila msimu. Lakini sasa
inataka zaidi.
Kichekesho zaidi,
klabu zinakatwa tayari fedha asilimia 6 katika mapato na zinakwenda kwenye
mfuko huo.
Kukata mapato ni
jasho lao, sawa hilo limekubalika, kukata hizo wanazopewa na wadhamini ndiyo juhudi
na morali, ni sawa na kuwaua kisoka. Hofu yangu, TFF isije ikaagiza hata
asilimia 5 za mishahara ya wachezaji na makocha nayo ianze kukatwa ili kusaidia
soka.
Vodacom:
Udhamini wa
Vodacom uko hivi, nitaufafanua kidogo; mkataba huo wa Vodacom uliosainiwa
Septemba 11, 2012 ni wa miaka mitatu na kila msimu unatofautiana.
Msimu wa 2012-13,
klabu zote 14 zilipewa Sh milioni 882 kwa ajili ya usafiri na zikigawanywa kila
moja inapata Sh milioni 63. Msimu wa 2013-14, zinatolewa Sh milioni 952 (kila
klabu Sh milioni 68) na msimu wa mwisho wa 2014-15 Vodacom wanatoa Sh bilioni
1.1 (kila timu Sh milioni 72).
Mgawo wa TFF kwa
fedha kutoka Vodacom katika misimu hiyo mitatu uko hivi; 2012-13 (Sh milioni
160), 2013-14 (Sh milioni 172) na 2014-15 (Sh milioni 183).
Ukichukua fedha
za TFF kwa kila msimu, toa za klabu moja, utagundua TFF inapata zaidi ya kila
klabu kama ifuatavyo. Msimu wa 2012-13 (TFF inapata zaidi Sh milioni 97),
2013-14 (zaidi Sh milioni 104) na 2014-15 ambao ndiyo msimu huu (TFF inachota
zaidi ya Sh milioni 111).
Kila msimu fedha
ya Vodacom imepanda kwa kila klabu, lakini pengo la kuchukua nyingi zaidi kwa
TFF nalo linazidi kuwa kubwa!
Azam TV:
Mkataba wa Azam TV, una pande tatu, kampuni hiyo ya runinga, TFF na Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPL). Kampuni hiyo inatoa fedha sawa kwa pande hizo mbili.
Mkataba wa Azam TV, una pande tatu, kampuni hiyo ya runinga, TFF na Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPL). Kampuni hiyo inatoa fedha sawa kwa pande hizo mbili.
Ni wa misimu
mitatu ukianza 2013-14, TFF na TPL kila moja inapewa Sh milioni 140, 2014-15
(kila mmoja Sh milioni 154) na 2015-16 (kila moja Sh milioni 169). Kwa misimu
yote mitatu, wote wawili, kila mmoja anapata Sh milioni 463.4.
Mgawo wa Azam TV
kwa kila klabu kwa misimu mitatu uko hivi, msimu wa 2013-14 (Sh milioni
100), 2014-15 (Sh milioni 110) na 2015-16 (Sh milioni 121). Jumla kwa misimu
yote mitatu, kila klabu italamba Sh milioni 331.
Msimu wa kwanza
TFF inazizidi klabu kwa Sh milioni 40, wa pili Sh milioni 44 na wa tatu Sh
milioni 48, maana yake pengo la wingi kati ya TFF pia linazidi kuongezeka kila
wadhamini wanavyoongezeka kama ilivyo kwenye ule mkataba wa Vodacom!
Kama umeona yote
hayo, basi nitakuachia maswali zaidi utafakari na kujiuliza, vipi TFF
hairidhiki? Vipi inataka kufanya dhuluma mchana na vipi haitaki kujibu hoja na
inafanya lazima?
Jiulize TFF na
klabu, ipi inalipa mshahara watu wengi, ipi inasafiri zaidi na ipi ina gharama
nyingi za uendeshaji, lakini usisahau shirikisho hilo kila mwaka linapewa dola
250,000 (zaidi ya Sh milioni 400) kwa ajili ya maendeleo ya soka kutoka kwa
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Usisahau TFF
inapata fedha za mfumo wa maendeleo ya soka kutoka kwenye makato ya viingilio
vya klabu na haijawahi kusema hata mara moja kwa mwaka inaingiza kiasi gani na
kinatumika vipi. Hakika inatakiwa kueleza hilo kwa kuwa fedha hizo ni za
taasisi ya umma na si ya Malinzi au washauri wake!
Kutaka klabu
ziwatangaze wadhamini, halafu fedha zitumike kuisaidia Taifa Stars, si sahihi.
Hii inaonyesha mawili.
Moja, fedha
inazopata TFF kutoka kwa wadhamini hazitumiki vizuri na wakati wa kuanika
mahesabu hadharani umefika sasa.
Pili, unaweza
kusema ukosefu wa ubunifu kwa kuwa TFF ina kitengo cha masoko ambacho
kingefanya kazi ya kusaka wadhamini ambao watakubali kuzidhamini timu za vijana
na watoto kama ambavyo uongozi wa Malinzi ulivyoingia madarakani na kuikuta
Taifa Stars tayari inadhaminiwa na Kilimanjaro, uongozi wa Tenga ulifanya ubunifu
ndiyo maana haukuingia kwenye mzozo na klabu kwa kutaka fedha zao za udhamini
ambazo zilikuwepo tokea wakati ule, ndiyo maana nasema uongozi wa sasa wa
Malinzi, umefeli. Nitarudi.
0 COMMENTS:
Post a Comment