October 6, 2014


NILIWAHI kuandika makala na kuelezea kuhusiana na suala la Simba kushindwa kufanya kwenye Ligi Kuu Bara kwa mechi mbili mfululizo.

Nilichokuwa nakipinga ni kuhusiana na zile hisia za zama za mawe, eti inashindwa kufanya vizuri kwa ajili ya laana ya kundi linalojulikana kama Simba ukawa.


Wako mashabiki au waliojiita wanachama wa Simba walihojiwa kwenye vyombo vya habari na kueleza jambo hilo, nikaona wanasambaza hisia ambazo si sahihi kwenye jamii.


Vizuri ilikuwa ni kuangalia vizuri mambo kiufundi, tena uwanjani na si kuyaangalia kishabiki kupindukia au kishirikina kwa hisia za kudhani, kitu ambacho si kizuri kwa dunia tunayoishi sasa.
Naendelea kupinga hisia hizo zisizo na mashiko za kuwa Simba haifanyi vizuri kwa sababu ya Simba ukawa. Ila nahimiza suala la umoja, kupatana, kurekebisha na kuelewana ni hema kwao kama Wanasimba.
Tukirudi kwenye kikosi cha Simba, juzi kimetopata sare ya tatu mfululizo na kuweka reokodi mpya ya kufululizo sare katika mechi za kwanza za ligi.

Mbaya zaidi mechi zote tatu iko nyumbani ikianza na sare ya mabao 2-2 dhidi ya Coastal Union, 1-1 dhidi ya Polisi Morogoro na juzi 1-1 ilipokutana na Stand United ya Shinyanga.
Usisahau Simba imeweka rekodi mpya ya kutoka sare mbili mfululizo dhidi ya timu mbili zilizopanda daraja, yaani Polisi Moro na Stand United, hii inaonyesha lazima jambo lifanyike.
Hali inavyokwenda na hasa katika mechi dhidi ya Stand unaweza ukasoma jambo miongoni mwa wachezaji wa Simba, kuwa kuna presha kubwa nyuma yao inayowasukuma, kwamba lazima wapate ushindi.
Kweli, viongozi wanaonekana wamechoka na sasa wanesukuma presha, huenda wanalazimika kwenda mazoezini na mazoezini ili kuhimiza wachezaji wao lazima washinde.
Bado utaona, Kocha Patrick Phiri hana raha, baada ya mechi dhidi ya Stand alitikisa kichwa, kuonyesha anaumia na hakubaliani na matokeo hayo.

Kutikisa kwake kichwa, kitu ambacho ni nadra kunaweza kutafsiriwa kwa hisia tofauti lukuki. Kwamba huenda amechoka, anashangazwa au anfikiria kuondoka na kurejea nyumbani kwao.
Kwani anajaribu kufundisha au kuelekeza kinachotakiwa, lakini inaonekana inashindikana na makosa ya aina moja yanajirudia katika mechi tatu mfululizo, kushindwa kuzitumia nafasi kufunga na kuruhusa mabao ya kusawazisha!

Kwa wanaojua rekodi zake, akichoshwa huwa anaanga na kuondoka zake kurejea kwao kimyakimya, hataki makuu. Yote yanawezekana ikawa anapinga presha kutoka kwa uongozi au vinginevyo.
Pia inawezekana akawa amechoshwa na malekezo yake kutofanyiwa kazi kama ambavyo amekuwa akitaka na wachezaji wake wamekuwa wakipoteza nafasi nyingi zaidi.
Ukipata nafasi rudia kuangalia mechi za Simba dhidi ya Coastal, Polisi Moro na Stand utaona Simba ndiyo timu inayoongoza hadi sasa kupoteza nafasi nyingi zaidi za kufunga.
Kuwa na bunduki bila ya risasi unaweza usiwe hatari, ukazidiwa na mwenye kisu. Ndiyo ilivyo Simba, ina uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi, lakini hakuna wenye uhakika wa kuitupia wavuni, ni kupoteza muda.
Inaonyesha maelekezo yote anayotoa Phiri yanafanya kazi ndiyo maana Simba imeweza kutengeneza nafasi nyingi zaidi za kufunga mabao, lakini wafungaji hakuna.
Kweli wachezaji wanataka wafundishwe kupita kiasi namna ya kuuweka mpira wavunini. Wangekuwa Watanzania pekee tungeingia kwenye hofu labda hatuna shule za kutosha ndiyo maana wanapata shida. Lakini kuna Waganda na Warundi, vipi sasa wanashindwa?
Tena rekodi zinaonyesha wako ambao wamefanya vema hapo kabla ya kufunga mabao mengi kama Emmanuel Okwi na Amissi Tambwe, sasa tatizo nini?
Nasisitiza, kusema eti Simba ina kikosi kichovu si sahihi, mpira wanaucheza tena mzuri, lakini wanatakiwa kufunga na ndiyo tatizo kubwa walilonalo.
Ndiyo maana nasisitiza suala la presha linaweza kuwa zuri lakini pia linaweza kuwa baya kwa Simba. Hivyo namna ya kuwahimiza wachezaji kunatakiwa kuwa na umakini mkubwa sana, la sivyo itakuwa ni kubomoa badala ya kujenga.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic