Kipa wa Costal Union ya Tanga,
Shabani Kado, amehuzunishwa na kifo cha aliyekuwa kipa wa timu inayoshiriki
Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Orlando Pirates na timu ya taifa ya nchi hiyo, Senzo
Meyiwa.
Senzo alifariki alfajiri ya juzi Jumatatu kwa
kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.
Kado amesema kuwa
ameshtushwa na kifo hicho cha ghafla cha mlinda mlango huyo ambapo kwa upande
wake alikuwa anamuangalia kama kipa ambaye atakuwa tishio hapo baadaye na
alikuwa anajifunza kupitia kwake.
Aliongeza kuwa, yeye kama mlinda mlango
ataendelea kumkumbuka kipa huyo na kwa kumuenzi, atahakikisha anafuata nyendo
zake kwa kukaa imara langoni.
“Kifo chake nimekipokea kwa masikitiko makubwa
kwani alikuwa ni mmoja wa walinda mlango waliokuwa wanakuja kwa kasi na
ataendelea kukumbukwa na wapenzi wengi wa soka hapa Afrika.
“Nitamuenzi kwa kuhakikisha nafuata
nyendo zake ambapo alipokuwa akikaa lango basi ilikulazimu ufanye kazi ya ziada
kuweza kumfunga,” alisema Kado.








0 COMMENTS:
Post a Comment