Na Saleh Ally
KUNA matatizo mengi ya kifundi
kwenye Ligi Kuu Bara na kinatakiwa kitengo cha ufundi kinachohusika na suala la
upangaji wa ratiba kuliangalia suala hilo.
Hii ni mara ya kwanza kwa
ratiba ya Ligi Kuu Bara kuwa kwenye mfumo wa mechi kuchezwa katika kipindi cha
wikiendi pekee.
Timu 14 za ligi hiyo, sasa
zinachuana siku mbili tu kwa wiki, maana yake kila timu inacheza mara moja kwa
wiki, sawa na mara nne kwa mwezi na si zaidi.
Ratiba hii inaweza
kuonekana sawasawa kama utaiangalia kwa haraka, huenda wataalamu wa Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania (TPL) waliamini iko sahihi bila
ya kuifanyia uchunguzi wa kina.
Lakini inawezekana ikawa
ratiba pekee ambayo ni nyanya na yenye makosa mengi inayoweza kuchangia
kushusha vitu vingi kisoka likiwemo suala la viwango vya uchezaji wa
Watanzania.
Kuna kila sababu ya
kuiangalia upya kwa kuwa itashusha viwango, itakimbiza wadhamini, inazipa timu
hasara na kadhalika.
Wachezaji:
TFF au TPL wanaweza kusema
hata England wanacheza mechi moja ya ligi kwa wiki na ziko timu ishirini, au
huenda waliiga huko, kitu ambacho kilikuwa ni kosa kubwa kwa mfumo wa soka ya
Tanzania.
Kwa timu 20 za England,
maana yake ligi inaweza kuchezwa kwa muda mrefu zaidi. Maana yake ni mzigo
mkubwa ukilinganisha na timu 14 za hapa nyumbani.
Wachezaji wao wanaweza kuwa
imara zaidi kutokana na wingi wa timu, lakini usisahau ligi yao ni ngumu, nzito
na haiwezi kufananishwa hata chembe na yetu.
Pia usisahau kwa England
kuna ligi tatu zinaendelea. Premier League, FA Cup na League Cup ambazo zote
zina kiwango cha juu na zinatoa makombe yanayotambulika na kuheshimika.
Hivyo hufikia wakati,
wachezaji wakacheza zaidi ya mechi tatu katika siku nane tu. Tanzania
mashindano ni ligi kuu tu!
Wadhamini:
Kila mdhamini hupenda
kutangazika, kumshawishi atoe mamilioni ya fedha lazima aone faida yake.
Ligi ikiendelea kuwa ya Jumamosi
na Jumapili pekee, itawakimbiza wadhamini wengi ambao hawatapenda bidhaa zao kupata
nafasi ya kutangazika mara moja tu kwa wiki au mara nne kwa mwezi.
Katika siku saba,
unatangazika mara moja tu, katika siku 30, unatangazika mara nne tu! Hii si
sawa na hauwezi kusema mdhamini wa ligi ya Tanzania atafaidika mazoezini pekee.
Yote yanawezekana na
yanaweza kuwa sehemu ya matangazo, lakini uwanjani timu inapocheza ligi ndiyo
sehemu namba moja.
Waajiri:
Klabu hasa Yanga, Simba na
Azam FC ambayo sasa ina tangazo la benki, zinalipa fedha nyingi kwa wachezaji
wake.
Kufanya kazi mara moja kwa
wiki ni sahihi? Mazoezi yanaweza kuwa kazi, lakini kuitumikia klabu mara moja
kwa wiki kuhakikisha inashinda linaweza kuwa jambo zuri kwa mwajiri?
Mwajiri makini angependa
kulipa vizuri na utumishi uwe wa juu na hasa kwa muda mwafaka, jiulize kwa kazi
ya dakika 90 kwa wiki nzima uwanjani mchezaji anaipigania timu, inatosha kwa klabu
kulipa mamilioni ya fedha?
Maana yake wachezaji
wanakuwa uwanjani kwa saa sita tu kwa wiki kuitumikia au kupambana kwa ajili ya
timu chini ya klabu yao!
Timu ya taifa:
Kwa mfumo wa kucheza mechi
sahihi ya ushindani kwa dakika 90, yaani saa moja na nusu kwa wiki nzima, vipi
unataka kutengeneza timu bora ya taifa?
Moja ni kutengeneza
wachezaji goigoi wanaojiandaa na mechi moja ya ligi kwa siku sita. Wanatumia
saa 144 yaani siku sita, kujiandaa na mechi ya saa moja na nusu. Hii si sahihi.
Kumbuka Taifa Stars ina
wachezaji wachache wanaocheza ligi za nje, hivyo tegemeo ni wachezaji kutoka
ndani ambao kama wataishi na mfumo huu wa mechi moja kwa wiki, haitakuwa rahisi
kuwa na timu bora ya taifa.
Pia ni tatizo kwa wachezaji,
mfano mchezaji alikuwa majeruhi wiki hii, halafu wakati anarejea ndiyo
Jumamosi, hakupata nafasi ya kucheza. Basi atasubiri wiki nyingine bila sababu
za msingi!
Katikati:
Kwa wachezaji wetu, jiulize
katikati ya wiki, hesabu siku sita kwa mchezaji mwenye mechi Jumapili, anakuwa
anafanya nini?
Mfumo wa ligi na ratiba
yake, unawafanya wachezaji kufikiria ligi ni rahisi na huenda hakuna ugumu kwa
kuwa kuna siku moja tu ya kucheza.
Wachezaji 30, kwa mechi 26
zinazochezwa kila baada ya siku 6. Hakika ni kuchangia kuua vipaji vya wengi
ambao mwisho wanakata tamaa na kuamua kufanya biashara ndogondogo, kumbe kama
mfumo ungekuwa mzuri, wangekuwa nyota wa baadaye na msaada kwa taifa letu. TFF,
TPL hata kama hamuelewani, badilisheni ratiba yenu, haina msaada kwa wachezaji,
klabu na hata wadhamini waliojitokeza na haitawashawishi wengine kuingia.
Mshika karamu,Jaribu kufikiria kabla ya kuandika,TFF tayari imeyarudisha mashindano ya FA ambayo yatakuwa yakipigwa katikati ya wiki hivyo kila timu kuna uwezekano wa kucheza mechi 2 kwa wiki na kuwafanya wachezaji wengi hasa wale wakaao benchi kucheza.
ReplyDeleteWakati hayo yanaelezwa na Rais wa TFF sisi viongozi wa Timu tulikuwepo na tulimuunga mkono haswa kwa suala la kutafuta mdhamini wa mitanange hiyo.Kama kitu hukifahamu ni bora ukauliza na si kuanza kuropoka.