Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), Mwesigwa Celestine , amesema kuwa malalamiko juu ya changamoto za mfumo
mpya wa matumizi ya tiketi za kielektroniki yamefika mezani kwake na
akasisitiza kuwa tayari wameanza kulifanyia kazi suala hilo.
Kumekuwa na malalamiko ya mfumo huo wa tiketi
ikiwemo kulanguliwa, pia kuwepo na mashine chache za kutolea huduma hiyo
uwanjani jambo linalofanya baadhi ya mashabiki kutoingia uwanjani kwa muda
muafaka kuzisapoti timu zao.
Mwesigwa amesema malalamiko juu ya mfumo huo
wameyapata na wameyafikisha sehemu husika ambapo ni CRDB ili kuweza kuyatafutia
ufumbuzi na kusisitiza kuwa tatizo hilo litamalizika katika michezo michache ya
hivi karibuni.
“Hili tatizo nikiri tu lipo maana malalamiko
yapo mengi na yametufikia walengwa, tulichokifanya ni kuwasiliana na watoa
huduma (CRDB) na kuwafikishia ambapo wametuhakikishia watalipatia ufumbuzi ndani
ya muda mchache tu, hivyo tunaomba tu mashabiki wawe na subira maana teknolojia
hii ni mpya hapa kwetu.
“Jambo jema ni kwamba CRDB wameonyesha ushirikiano
mkubwa katika hilo na kuahidi ‘kuimprove’ huduma yao ili wadau wa soka
waendelee kuona burudani na kuzisapoti timu zao bila tatizo,” alifafanua
Mwesigwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment