Klabu ya Azam FC imegoma kutoa kitita
cha dau la usajili dola 15,000 (sawa na shilingi milioni 26) kwa ajili ya
kumsajili kiungo wa Simba, Amri Kiemba katika usajili wa dirisha dogo msimu
huu.
Kauli hiyo imekuja siku chache tangu Azam FC ilipojibiwa
barua na Simba ya kumtaka kiungo huyo kwa mkopo katika usajili wa dirisha dogo
msimu huu lililofunguliwa Novemba 15, mwaka huu.
Azam FC ndiyo ilianza kuandika barua ya
kumuomba kwa mkopo Kiemba ikiwa ni siku chache tangu asimamishwe na uongozi wa
timu hiyo pamoja na wenzake, Shaaban Kisiga na Haroun Chanongo.
Katibu Mkuu
wa Simba, Stephen Ally, alisema wamepokea barua ya majibu kutoka Azam FC hivi
karibuni ya kukataa kutoa kiasi hicho cha fedha huku ikisisitiza kumuomba kwa
mkopo.
Stephene alisema mara baada ya kupokea barua
hiyo, amepanga kupeleka suala hilo kwenye Kamati ya Utendaji ya timu hiyo
ambayo itatoa majibu sahihi kuhusiana na hatma yake.
“Tunashukuru tumepokea barua ya majibu kutoka
Azam FC hivi karibuni juu ya kumhitaji Kiemba katika usajili wa dirisha dogo
baada ya kumuomba kutuandikia barua ya kumhitaji kwa mkopo.
“Sisi katika majibu yetu tuliwaambia hatupo
tayari kumuachia kwa mkopo Kiemba na badala yake watupatie dola 15,000 za
usajili ili tumuachie aende akaichezee Azam FC ambayo imeonyesha nia ya
kumsajili,” alisema Stephen.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Azam FC, Said
Mohamed kuzungumzia hilo, alisema: “Hatupo tayari kutoa fedha yoyote kwa ajili
ya kumsajili Kiemba, sisi tulimuomba kwa mkopo mchezaji na siyo kumnunua moja
kwa moja, wenyewe kama hawataki basi.”
0 COMMENTS:
Post a Comment