Kocha wa Simba Mzambia, Patrick Phiri,
ameibuka na kudai kuwa atamkumbuka kiungo wake Amri Kiemba iwapo atakamilisha
dili lake la kutimkia Azam FC ambayo inamuwinda kwa mkopo.
Kiemba anadaiwa kutakiwa na Azam FC kwa mkopo,
baada ya kutoelewana na uongozi wa Simba ambao ulikuwa ukimtuhumu mara kwa mara
kucheza chini ya kiwango wakati akiitumikia klabu hiyo tofauti na anapokuwa na
timu ya taifa, Taifa Stars.
Kutokana na hali hiyo uongozi wa Simba ulimsimamisha
pamoja na wachezaji wenzake wawili ambao ni Shabani Kisiga na Haruna Chanongo.
Phiri alizungumza na SALEHJEMBE akiwa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, tayari kwenda Zambia na kusema iwapo ataondoka, atamkumbuka sana kiungo huyo ambaye alifanya naye kazi akiwa Simba.
Alisema anatamani kuona anaendelea kuwa naye
kwenye kikosi chake lakini wenye maamuzi ya mwisho ni viongozi wa timu hiyo.
“Kiemba ni mchezaji mzuri ambaye katika
kipindi chote alichokuwa na mimi sikuwahi kugombana naye, hivyo nitammisi sana
katika kikosi changu iwapo ataondoka lakini naamini kwa uwezo wake anaweza
kufanya vizuri popote atakapokwenda.
“Kuhusiana na kuziba pengo lake nimeshaongea
na viongozi, pia katika ripoti yangu hilo nimelizungumzia, ni matumaini yangu
kuwa litafanyiwa kazi na tutampata mbadala wake,” alisema Phiri ambaye
anatarajia kurejea nchini Novemba 26 mwaka huu kuendelea na majukumu yake ya
kukinoa kikosi hicho chenye maskani yake mtaa wa Msimbazi.
0 COMMENTS:
Post a Comment