Usajili mpya wa Yanga hautafanyika hadi kocha wake mkuu, Marcio
Maximo, atakaporejea nchini baada ya Novemba 20.
Maximo ameitaka Kamati ya Mashindano ya Yanga inayohusika na
usajili, kuvuta subira hadi atakaporejea.
“Kweli kocha ameomba kamati imsubiri na yeye ndiye mwenye
mapendekezo ya mchezaji yupi anamtaka. Ili usajili uanze, lazima aanze kukaa na
kamati, awape ripoti yenye mapendekezo yake na baada ya hapo ndipo usajili
ufanyike,” kilieleza chanzo.
Tayari Maximo yuko kwao nchini Brazil ambako amekwenda kwa mapumziko
ya siku 10.
Yanga imeanza kufanya usajili wake kitaalamu zaidi, hivyo kamati
inayohusika na usajili itashirikiana na kiongozi wa benchi la ufundi kwa
ukaribu zaidi.
Tayari taarifa zinaonyesha Yanga inahitaji kuongeza viungo wawili
wachezeshaji kwa lengo la kutengeneza nafasi nyingi za kufunga. Haijajulikana,
Maximo atawapendekeza viungo gani wa ndani au yupi kutoka nje ya Tanzania.
Simba na Azam FC, tayari wameanza mikiki ya usajili kwa kuongeza
mikataba ya baadhi ya wachezaji na kusajili wapya.
0 COMMENTS:
Post a Comment