November 12, 2014



Na Saleh Ally
MJI wa Bujumbura una watu 497,166 kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka 2008. Hata kama kutakuwa na ongezeko hadi sasa, haliwezi kuwa zaidi ya 200,000.


Bujumbura ni mji mkuu wa nchi ya Burundi, mmoja ya miji mikuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki unayoweza kusema inaongozwa na Tanzania iliyolala.

Tanzania ndiyo nchi kubwa kuliko zote zilizo katika jumuiya hiyo, unaweza kusema inaaminika na ndiyo inachukua nafasi ya uongozi wa mambo mengi. Lakini sasa Kenya, Rwanda na Burundi zimeshika hatamu.

Lengo si siasa hapa ila nikukumbushe, Burundi ndiyo mji aliozaliwa mshambuliaji hatari wa kikosi cha Wes Brom inayoshiriki Ligi Kuu England ‘Premier’.

Jina la Saido Berahino haliwezi kuwa geni kwako, kinda wa miaka 21 ambaye sasa ni tishio katika Ligi Kuu England. Katika mechi 11 tayari amepiga mabao saba na anaonekana kuendelea zaidi.

Uongozi wa Wes Brom, umeamua kumuongezea maslahi. Tayari analipwa pauni 12,000 (Sh milioni 31) kwa wiki na mazungumzo ya kumuongezea zaidi yanaendelea huku Tottenham na Liverpool zikiwa zimetoa macho.

Berahino ambaye amezaliwa Bujumbura, anakwenda kuwa tishio England. Ukiangalia nchi zote za Afrika Mashariki na Kati, zina wachezaji wanaocheza kwenye ligi kubwa tano za Ulaya, yaani England, Hispania, Ujerumani, Italia na Ufaransa.

Ndiyo, hata kama ni mchezaji tu ambaye unaweza kumuita asili yake ni DR Congo, Rwanda, Uganda, lakini hakuna kutokea Tanzania ukiachana na Adam Nditi ambaye bado hajapanda kwenye kiwango cha ligi hizo na hajafika mbali!

Jamani, Rwanda, Burundi nao wanatoa wachezaji. Kama kigezo kingekuwa wingi wa watu, basi Tanzania ingekuwa na nafasi kubwa zaidi kwa kuwa kuliko na watu wengi ni rahisi kufanya uchekechaji wa kupata kitu bora.

Hata utulivu pia kinaweza kikawa kigezo bora zaidi. Angalia nchi zote za Afrika Mashariki na Kati, yenye sifa na amani kuliko zote ni Tanzania.

Kama Bujumbura imetoa wachezaji, vipi Dar es Salaam yenye wakazi zaidi ya milioni nne inashindwa kuwa na mchezaji hata mmoja. Vipi mikoa mingine mingi ya Tanzania yenye vipaji lukuki?

Wakenya wana wachezaji waliocheza au wanacheza ligi zote kubwa. Italia, England na Ufaransa. Tanzania haina hata mmoja? Ukisema uhame kwenye soka, wao wako vizuri zaidi kwenye riadha.

Hata ule mchezo wa rugby ambao unaonekana ni wa Wazungu au kriketi unaoonekana ni wa Wahindi, wao wameshiriki hadi Kombe la Dunia. Waungwana, hapa kwetu Tanzania kuna nini? Nani mwingine anajiuliza hili?

Lazima tukubali kuwa kuna tatizo na kuna mambo mengi ya kuyafanyia kazi. Huu ndiyo wakati mwafaka wa kuamka na tusikubali, Watanzania tumelala na sehemu nyingi tulizoamka tunaendekeza majungu na ubinafsi.

Ubinafsi unajumuisha kujifikiria mwenyewe, kutokuwa mwenye utaifa na ambaye unajali kufanikiwa au kupata wewe peke yako hata kama wengine watakosa hata kidogo.

Mimi nasema wazi, mfumo wa uongozi kuanzia kwenye vyama, mashirikisho, klabu zetu ni tatizo. Nchi yetu ina watu wengi mno wazembe ambao wanataka kuishi kwa kuombaomba.

Nianze na viongozi, TFF na Chama cha Riadha Tanzania (AT), wanaweza kuwa mfano mbaya zaidi kwa kuwa si watu wanaotaka maendeleo badala yake wanataka maendeleo yao binafsi.

Mbaya zaidi kama TFF, wameanzisha mfumo wa kijinga kabisa. Kwamba mtu akiwapinga jambo, basi anakuwa adui na wanaanza kumfanyia vituko.

Maana yake wanatumia nguvu na wanakoendea ni kubaya na wanaufanya mpira wa Tanzania uwe katika ule mfumo wa “Chukua chako mapema”, anayeingia kwenye njia hiyo, hakika ni mzalendo na hawezi kupinga kuwa ni mbaguzi.

Mfumo wa maendeleo ya michezo yetu umejaa malumbano kwa kuwa hauna viongozi wanamichezo. Wengi wao wanataka kuchuma ndani ya michezo na si kuiendeleza.

Vipaji tunavyo lukuki hata kuliko Burundi, Rwanda na kwingineko. Wanaovimaliza na kuvizika vikiwa hao ni viongozi kama wale wa TFF na AT. Hakuna anayejali, hakuna anayejua na hawana habari kwa kuwa wote wanajikumbuka au wanawaza maisha yao binafsi.

Hakuna mipango yoyote ya kuvumbua vipaji, kuviendeleza na kuvipa nafasi. Mbaya zaidi hata wale waliokuwa makomandoo, wenye tabia ya ombaomba, leo wanaweza kuingia na kuongoza kwenye shirikisho kubwa kama hilo la soka. Haya ni mauaji ya soka na michezo mingine.

Berahino atatokea vipi Dar es Salaam au mikoa mingine ya Tanzania wakati kila kitu kimeuawa. Mungu tusaidie, viongozi wasio wazalendo kama hawa waone haya, wachoke, wajisikie vibaya na mwisho wawaachie wale wenye nia ya kuisaidia Tanzania iendelee.

Wengine tunaumia kwa kuwa tunaona fedha zinaliwa na ‘wajanja’ hao wachache, huku nchi yetu ikishindwa na kila nchi iliyo kwenye ardhi hii ya dunia uliyoiumba, tusaidie tafadhali.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic