Uongozi wa timu ya Ndanda FC ya mkoani Mtwara,
upo katika harakati za kusajili wachezaji sita kwa ajili ya kuimarisha kikosi
chao kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu Bara.
Timu hiyo ambayo ilipanda ligi kuu msimu
uliopita, imeonekana kusuasua katika ligi hiyo kwa kucheza michezo saba na
kufanikiwa kushinda miwili huku ikifungwa mitano na sasa ipo katika nafasi ya
13 baada ya kujikusanyia pointi sita kwenye msimamo wa ligi.
Kocha wa timu hiyo, Abdul Mingange, alisema
ameshakabidhi ripoti yake kwa uongozi wa timu hiyo baada ya kucheza michezo
miwili kufuatia kutimuliwa kwa kocha aliyeipandisha ligi kuu, Dennis Kitambi
ili kuipitia na kuona upungufu uliopo.
Alisema nafasi zinazotakiwa kufanyiwa usajili
kwa timu hiyo ni kipa, beki, kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji na
mshambuliaji kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho ili kuweza kufanya
vizuri katika michezo inayofuata.
“Tunatarajia kufanya usajili wa wachezaji sita
ili kuweza kuimarisha nguvu kwenye kikosi ili kuziba upungufu uliopo na
kupigania ushindi kwenye ligi kwa ajili ya kushika nafasi za juu,” alisema
Mingange ambaye ni meja mstaafu wa Jeshi la Wananchi.
0 COMMENTS:
Post a Comment