Azam FC Imetamka kuwa haipo tayari kumuachia
beki wao wa kati, Said Morad kujiunga na Simba inayomhitaji katika usajili wa dirisha
dogo katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
Kauli hiyo imetolewa ikiwa ni siku chache baada ya
kuwepo na tetesi za Simba kuomba kubadilishana na beki huyo na kiungo
mshambuliaji mkongwe wa Msimbazi, Amri Kiemba aliyesimamishwa na uongozi wa
timu hiyo.
Awali, Azam FC ndiyo iliyoanza kumuomba Kiemba kwa mkopo
baada ya uongozi wa Simba kumfungia pamoja na wenzake, Shaaban Kisiga na Haroun
Chanongo kwa kile kilichodaiwa utovu wa nidhamu waliouonyesha wakiwa Mbeya
wakijiandaa na mechi dhidi ya Tanzania Prisons.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Mwenyekiti wa Azam
FC, Said Mohamed, alisema hawatakubali kumuachia beki huyo kutokana na
kumhitaji, licha ya kumsajili beki mwingine Muivory Coast, Serge Wawa
aliyetokea El-Mereikh ya Sudan.
Said alisema, wao wamemuomba Kiemba pekee katika usajili
wao baada ya kupokea mapendekezo ya kocha wao Mcameroon, Joseph Omog kutokana
na aina ya kiungo anayemhitaji katika kukiimarisha kikosi chake na siyo
kubadilishana.
Aliongeza kuwa, Simba kama hawataki kumtoa kwa mkopo
Kiemba basi, lakini siyo kubadilishana, hivyo beki atabaki kuendelea kuichezea
timu hiyo katika raundi ya nane ya ligi kuu iliyosimama.
“Sisi tulimuomba Kiemba kwa mkopo na siyo kumnunua kwa
jumla na beki wetu Morad haendi popote, atabaki kuendelea kuichezea Azam FC
kutokana na kuwepo kwenye mipango na kocha wetu Omog,” alisema Said.
Imeelezwa pamoja na kuwa na mabeki wengi wa kati, Azam FC imeonekana haina uhakika kama Serge Wawa iliyemsajili kutoka Sudan atazoea haraka mazongira ya Tanzania.
Hivyo itaendelea kubaki na Morad, halafu itaangalia kama inaweza kumuachia mwishoni mwa msimu.
0 COMMENTS:
Post a Comment